MALAIKA WA MUNGU - SEHEMU YA TATU


 NAMNA KADHAA MALAIKA WANAVYOTENDA KAZI ZAO

1. Malaika wa Mungu wanaweza kutenda kazi zao waziwazi au kwa namna isiyo ya wazi. Kutenda kazi waziwazi namaanisha Malaika anatokea unamuona Kwa macho ya damu na nyama, unazungumza naye, anakupa maelekezo au anazungumza na wewe waziwazi kama ilivyokuwa kwa Mtume Petro (Matendo ya Mitume 12:7-11), Gideoni (Waamuzi 6:11-12) nakadhalika.

2. Malaika wa Mungu wanaweza kutenda kazi zao kupitia mawazo au fikira, kuweka msukumo au mguso ndani ya mtu ili mtu afanye jambo Fulani nakadhalika.

(Mwanzo 24:7-27)

Ibrahimu alimwambia mtumishi wake kuwa "Malaika wa Mungu atakutangulia ili umpate mwanamke ambaye ataolewa na Isaka"

Ukweli ni kwamba Malaika hakuwa anaonekana ila alikuwepo, yule mtumishi akaondoka akafika mpaka kwenye kisima Fulani akasema "binti atakayenipa maji ninywe na kunywesha ngamia huyo ndiye atakuwa mke wa Isaka"

Alipomaliza kuwasilisha maombi hayo Kwa Mungu wa Ibrahimu ghafla Rebeka anatokea, akaombwa maji akampa akanywesha na ngamia, MALAIKA ALIYETANGULIA MBELE YA MTUMISHI HUYO NDIYE ALIWEKA MSUKUMO HUO NDANI YA REBEKA AKAWA TAYARI KUMPA YULE JAMAA MAJI NA AKAWA TAYARI KUNYESHA NA NGAMIA.

3. Malaika wa Mungu wanaweza kuja kutenda kazi zao kama wageni wanaokuja kukutembelea au wanaweza kuja kama wanadamu na mkakutana njiani.

(Waebrania 13:2)

Biblia imeweka wazi kuwa mtu anaweza kupokea au kukutana na Malaika bila yeye kujua kuwa amepokea Malaika au amekutana na Malaika au anaongea na Malaika wa Mungu, ndio maana Biblia inasema ni vema kupokea wageni.

4. Malaika wa Mungu wanaweza kufanya Kazi zao kupitia ndoto na maono.

Tofauti ya ndoto na maono ni hii, maono unaona ukiwa haujalala yaani macho yako ya ndani yanafunuliwa unaanza kuona mambo ya rohoni. Ndoto ni mlango unaofunguka mwanadamu akiwa amelala iwe mchana au usiku maadamu Uwe umelala (ni vema ufahamu kuwa kulala ni ufunguo wa mlango unaoitwa ndoto)

(Mathayo 1:20

Yusufu alitokewa na Malaika katika ndoto alipokuwa amelala.

(Matendo ya Mitume 10:3-4)

Kornelio alimuona Malaika kupitia maono.


Angalizo: Ni vema kupokea wageni ila ni vema Zaidi Kumsikiliza Mungu anakuongozaje kwa kila mgeni unayempokea.

Mungu akubariki Kwa hayo machache naamini umejifunza mengi sana, endelea kuniombea Mungu anipe mengi Zaidi ya kukushirikisha.

Hapa ndipo somo letu linafikia mwisho Kwa Awamu hii ya Kwanza, maombi yako yanaweza kusababisha Awamu zingine zikaja, hivyo basi endelea kuniombea.


Chapisha Maoni

0 Maoni