✍️Faraja Gasto
Mungu hutuwazia mawazo mema kila wakati haijalishi ni wakati wa raha au wakati wa taabu (Yeremia 29:11)(Isaya 55:8-9), Mungu anawaza mema kwa ajili ya watu wote haijalishi ni wema au waovu.
Wakati wa taabu ni wakati ambao hauoni wa kukusaidia, umekata tamaa, unapitia kipindi kigumu kiuchumi, kisaikilojia, kimahusiano nakadhalika.
Hata katika wakati wa taabu Mungu huachilia mawazo yake ndani ya watu ili yawasaidie na kuwafanikisha katika mambo mbalimbali lakini si wengi ambao hutendea kazi mawazo hayo. Mawazo ya Mungu yanayokujia katika nyakati mbalimbali ikiwemo nyakati za taabu ni muhimu sana uyatendee kazi Kwa kuwa yamebeba msaada mkubwa kwa ajili yako na kwa ajili ya wengine.
Nataka nikutazamishe mifano michache ya watu ambao waliyatendea kazi mawazo ya Mungu yaliyowajia wakati wa taabu.
MFANO WA 1: WENYE UKOMA WANNE
(2 Wafalme 7:3)
Hawa wakoma walikuwa kwenye wakati mgumu sana lakini ghafla Kuna wazo lilikuja kama swali "mbona tunakaa hapa hata tufe?"
Hilo wazo liliwafanya wakatoka pale walipokuwa wakaenda Kwa maadui zao, wakati wanakwenda Mungu alifanya jambo la ajabu sana, lile wazo walipewa na Mungu walipolitendea kazi maisha yao yalibadilika.
MFANO WA 2: KIJANA ALIYETAPANYA MALI (MWANA MPOTEVU)
(Luka 15:11-24)
Huyu kijana alipokuwa kwenye wakati mgumu Kuna wazo lilimjia ghafla kama swali "ni watumishi wangapi Kwa baba yangu wanakula na kusaza na mimi hapa ninakufa kwa njaa" likaja wazo la pili lililompa mbinu, wazo lilimuongoza kutubu kwa kurudi Kwa babaye na kuomba msamaha.
Hilo wazo lilikuwa la Mungu, Biblia inasema "alipozingatia moyoni mwake" maana yake alipozingatia wazo lililoingia moyoni mwake maisha yake yalibadilika.
MFANO WA 3: MALKIA ESTA
(Esta 4:15-17)
Wakati wayahudi wamepangiwa tarehe ya kuuawa walijikuta wako kwenye kipindi kigumu sana, walilia kwa uchungu sana.
Katika kipindi hiki ndipo Esta alipata wazo la watu kufunga na kuomba kwa muda wa siku tatu ili wamuombee aweze kuingia kwa Mfalme Ahasuero kinyume na utaratibu.
Wazo hilo lilitoka kwa Mungu likaingia moyoni mwa Esta, wayahudi walipolitekeleza wazo hilo wanafanya maombezi kwa ajili ya Malkia Esta ndipo kukawatokea wokovu, aliyekusudia wauawe akauawa yeye mwenyewe (Esta 7:10)
NB: Nimekutazamisha mifano hiyo michache ili uelewe namna Mungu anavyojali watu wake, namna anavyoachilia mawazo yake Kwa watu hata wanapopitia vipindi vigumu na namna mawazo ya Mungu yalivyobadilisha maisha ya watu walioyatendea Kazi.
0 Maoni