LAITI UNGELIJUA


                      ✍️Faraja Gasto

Jambo mojawapo linalosababisha watu wengi wasipate mema ni DHARAU, dharau ni mbaya sana imewakosesha watu wengi mambo mema kama vile miujuza, misaada, kibali, kazi kuoa, kuolewa nakadhalika.

Wengine walipotambua madhara ya dharau ndio maana ilifika hatua wakasema "USIMDHARAU USIYEMJUA" na hata kama unamjua "USIMDHARAU KWA KUWA HUJUI KESHO YAKE, HUJUI ALICHONACHO, HUJUI ANACHOJUA, HUJUI ANAOWAJUA"

(Yohana 4:9)

"Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu nami ni mwanamke Msamaria?" 

Ukichunguza jibu la mwanamke Msamaria utaona lilikuwa na dharau ndani yake, sasa ona Yesu alichomwambia yule mwanamke "kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye nipe maji ninywe ungalimwomba yeye naye angalikupa maji yaliyo hai" (Yohana 4:10)

Yule mwanamke aliposikia jibu hilo alipatwa na mshangao akatamani kufahamu ni maji gani ambayo akinywa hawezi kuona kiu tena.

Ninachotaka uone hapo ni namna dharau inavyosababisha watu wengi kukosa mema, unadhani yule mwanamke angeanza kumtukana Yesu kisha akaondoka zake bila kumsikiliza Yesu je! maisha yake yangebadilika? JIBU JEPESI NI KWAMBA MAISHA YAKE YASINGEBADILIKA, angeendelea kuchukua Waume za watu kama ilivyokuwa kawaida yake.

NB: Ni mara ngapi kuna watu umewapuuza haukutaka kuwasikiliza? ulipowatazama ukaona hawana hadhi ya kuongea na wewe lakini LAITI UNGEJUA HUYO ULIYEKATAA KUMSIKILIZA NDIYE ANGEBADILI MAISHA YAKO, NDIYE ANGEKUPA MAWAZO YA KUKUFANIKISHA, NDIYE ANGEKUUNGANISHA NA WATU WA MUHIMU SANA KWAKO, NDIYE ANGEKUWA MUME AU MKE MWEMA KWAKO, NDIYE ANGESABABISHA UPATE KAZI NAKADHALIKA. 

(2 Wafalme 5:1-15)

Naamani alikuwa jemedari wa jeshi la Shamu (CDF - Chief of Defence Forces) lakini alikuwa na ukoma, wakati washami walipopigana na waisraeli waliteka binti mmoja akaletwa kumhudumia mke wa Naamani, siku moja binti yule alimpa taarifa mke wa Naamani kuhusu namna Naamani anavyoweza kupona ukoma.

Naamani alipotendea kazi taarifa ya binti yule hatimaye Naamani alipona ukoma uliokuwa ukimtesa.

NB: Mara ngapi umewapuuza watu unaowazidi cheo, unaowazidi umri, unaowazidi kipato, unaowazidi elimu nakadhalika? LAITI UNGEJUA HUYO ULIYEMDHARAU NDIYE ANGEKUPA MWANGA KUHUSU NAMNA YA KUFANIKIWA ZAIDI, NAMNA YA KUTATUA MATATIZO YANAYOKUKABILI NAKADHALIKA.

(1 Samweli 17:42-45)

Goliathi alipomtazama Daudi akamdharau akajisemea moyoni "yaani haka katoto nitakachanachana vipande halafu nyama yake nitawapa ndege wa angani na Wanyama WA mwituni" lakini LAITI GOLIATHI ANGEJUA MTU ANAYEKWENDA KUKABILIANA NAYE NI MTU WA AINA GANI, GOLIATHI ANGEKIMBIA KUEPUKA MATATIZO (DHARAU ILIMPONZA HATIMAYE AKAFA)

NB: Ni mara ngapi umemdharau mtu ukaona hana la kukufanya, hata ukimfanyia chochote hakuna wa kukusumbua halafu ghafla unakuja kugundua huyo mtu yuko tofauti na ulivyomchukulia? LAKINI LAITI UNGEJUA NI NANI HUYO UNAYEMUONYESHA JEURI.

NAKUSISITIZA: Epuka dharau.

°°°°Ni kweli hana pesa lakini anamjua Mungu na ana vitu vya kukupa.

°°°°Ni kweli hana elimu lakini ana imani inayoweza kukusaidia.

°°°°Ni kweli hana umbo namba nane lakini ana hofu ya Mungu.

°°°°Ni kweli havutii lakini haujui Kesho yake.

°°°°Ni kweli unamzidi elimu lakini anakuzidi akili.

°°°°Ni kweli ni maskini lakini ana taarifa nyeti za kukusaidia.

°°°°Ni kweli ni kapuku lakini anamjua mtu anayeweza kukusaidia.

°°°°Ni kweli hana nguvu lakini Mungu kwake ni kimbilio na nguvu.


Chapisha Maoni

0 Maoni