KIONGOZI MWENYE UWEZO MKUBWA WA KUFIKIRI


                      ✍️ Faraja Gasto


(Yoshua 1:8)


Kwa mujibu wa Biblia, sifa mojawapo ya kiongozi mzuri ni kwamba anatakiwa awe na uwezo mkubwa wa kufikiri (uwezo mkubwa wa kufikiri ni uwezo mkubwa wa kupima mambo kabla ya kufanya maamuzi) kwa manufaa yake na kwa manufaa ya anaowaongoza ndio maana Mungu alipomuita Yoshua na kumpa jukumu la kuongoza wana wa Israel, Mungu alimwambia "kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako bali UYATAFAKARI MANENO YAKE mchana na usiku" (Yoshua 1:8).


Kwa mantiki hiyo ni kwamba huwezi ukawa kiongozi mzuri ikiwa una uwezo mdogo wa kufikiri, ili uwe kiongozi mzuri lazima ujitahidi sana kuongeza uwezo wako wa kufikiri kwa sababu zifuatazo (hizi ni baadhi ya sababu)

1. Maamuzi utakayoyaamua yatakugusa wewe na unaowaongoza, ikiwa ni maamuzi mabaya yatakuathiri wewe na unaowaongoza.


2. Kuna mashauri mengi utayapokea ukiwa kiongozi, utapewa mashauri mema na mabaya, uwezo mkubwa wa kufikiri utakusaidia kuyapima mashauri na kuamua kwa usahihi.


MAMBO YA KUFANYA ILI UONGEZE UWEZO WA KUFIKIRI

1. Soma neno la Mungu sana (Biblia)

(Yoshua 1:8)

 Yoshua aliambiwa asome kitabu cha torati pia atafakari yaliyoandikwa humo, Iko hivi zamani zile kitabu cha torati ndicho kiliwasaidia viongozi, makuhani na watu binafsi kumjua Mungu, Kujua sheria, maagizo ya Mungu nakadhalika lakini nyakati hizi tuna Biblia, Kwa hiyo soma sana Biblia tafakari yaliyoandikwa humo.


2. Soma sana vitabu mbalimbali 

Mtume Paulo alipokuwa akimwandikia Timotheo nyaraka za kiuongozi, jambo mojawapo  alimwambia "FANYA BIDII KATIKA KUSOMA" (1 Timotheo 4:13). Hata Mtume Paulo alikuwa msomaji wa vitabu (2 Timotheo 4:13)


3. Omba hekima ya Mungu

Kazi mojawapo ya hekima ya Mungu ni kuongeza uwezo wako wa kufikiri ndio maana hekima ya Mungu ikiachiliwa ndani yako au ikiongezeka ndani yako utajikuta unakuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, hekima ya Mungu ikipungua ndani yako utajikuta unakuwa na uwezo mdogo wa kufikiri.


NB: Uwezo wa kufikiri ni uwezo wa kupima mambo kabla ya kufanya maamuzi.


Soma mifano michache ifuatayo kuhusu uhusuano wa hekima ya Mungu na uwezo wa kufikiri


(Mithali 6:6-8)

Biblia inampa ushauri mtu mvivu Kwa kumwambia hivi "ewe mvivu mwendee chungu ZITAFAKARI NJIA ZAKE UKAPATE HEKIMA" 


Biblia inataka tufahamu kuwa mvivu ana uwezo mdogo wa kufikiri, uvivu unapunguza uwezo wa kufikiri, uwezo mdogo wa kufikiri ni matokeo ya uvivu pia uvivu ni matokeo ya kukosa hekima. Kwa hiyo ili mtu aongeze uwezo wake wa kufikiri anatakiwa apate hekima ndio maana nimekuambia Kazi mojawapo ya hekima ni kuongeza uwezo wa kufikiri.


(1 Wafalme 3:128)

Mara baada ya Mfalme Sulemani kupewa hekima na Mungu, Mfalme Sulemani alijikuta amepata uwezo mkubwa wa kufikiri, siku moja akaletewa kesi ili aamue, kiuhalisia ukisoma kesi Ile ilikuwa kesi ngumu sana kuiamua lakini kutokana na hekima ya Mungu iliyokuwa ndani ALIYAPIMA maneno ya mshitaki na mshitakiwa na akapambanua yupi ni mwenye haki yupi hana haki. Kama Mfalme Sulemani angekuwa na uwezo mdogo wa kufikiri asingeweza kuiamua Ile kesi.


NB: Kwa mujibu wa Biblia chanzo kimojawapo cha kuchelewa Kwa hukumu za kesi ni mahakimu au Majaji kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri na hiyo inasababishwa na kukosa hekima ya Mungu Kwa hiyo kumbuka kuwaombea hekima.


Barikiwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni