Mambo ya kujifunza Katika fundisho hili
1. Aina za uinjilisti.
2. Baadhi ya mbinu za uinjilisti.
3. Mambo yanayosababisha uinjilisti Uwe na nguvu au ufanisi.
4. Mambo ya kuzingatia Katika uinjilisti.
5. Faida chache za uinjilisti.
Utangulizi
Lengo kuu la fundisho hili ni kuaandaa washuhudiaji wa habari njema za Yesu Kristo wenye maarifa ya ushuhudiaji Kwa Mujibur wa Biblia.
Ijulikane kuwa kila mtu aliyemwamini Yesu Kristo ana wajibu wa kufanya uinjilisti Kwa kuwa hilo ndilo agizo kuu (Marko 16:15-16)
Haijalishi wewe ni Mtume, mwalimu, nabii, mchungaji, mwinjilisti, mwimbaji au muumini Una wajibu wa kuhubiri injili.
Angalizo: Yesu hakututuma tuwashawishi watu watoke Katika makanisa yao bali ametutuma tuwaambie watu habari njema waje kwake.
UINJILISTI NI NINI?
1. Ni kueneza habari njema za Yesu Kristo au ni kutangaza habari njema za Yesu Kristo (Warumi 10:15)
2. Ni kushuhudia jinsi unavyomfahamu Yesu au ni kuwaeleza watu jinsi unavyomfahamu Yesu Kristo ( Yohana 4:28-32,39)
3. Ni kushuhudia yale ambayo Yesu alikutendea au Yale mambo ambayo Yesu amefanya Katika maisha yako ( Marko 5:19-20)
AINA ZA UINJILISTI
1. UInjilisti wa mtu kwa mtu au uinjilisti wa uso Kwa uso (Yohana 1:44-50)
Yaani unamfuata mtu halafu unamueleza habari za Yesu Kristo.
2. UInjilisti wa nyumba kwa nyumba (Matendo ya mitume 20:20-21)
Yaani unawafuata watu majumbani mwao halafu unawaeleza habari za Yesu Kristo.
3. UInjilisti wa mikutano au uinjilisti Katika makusanyiko ya watu (Matendo ya mitume 8:4-8) (Matendo ya mitume 2:1-41)
4. UInjilisti Kwa njia ya vyombo vya habari kama vile radio, runinga, vipeperushi, mango nakadhalika.
5. UInjilisti Katika taasisi za elimu kama shule na vyuo.
BAADHI YA MBINU ZA UINJILISTI
1. Kuwa nuru na chumvi (Mathayo 5:13-16)
Maisha yetu au mienendo yetu unaweza kuwafanya watu kuja Kwa Yesu au kutokuja Kwa Yesu ndio maana tunapaswa kuishi sawasawa na miongozo ya neno la Mungu.
2. Kujenga urafiki au kujiweka karibu na watu ambao hawajaokoka (Mathayo 9:9)
Yesu aliitwa rafiki wa wenye dhambi lakini Yesu hakuiga matendo yao bali alijiweka karibu na watu ambao hawajamwamini ili kuwahubiri injili.
Urafiki au ukaribu unaweza kumfanya mtu akawa tayari kukusikiliza ndio maana Yesu alijiweka karibu na watu ambao hawajamwamini.
3. Kwenda kushuhudia (Marko 5:19-20)
Yesu anataka uwaambie wengine ushuhuda wako kuhusu namna alivyokutana na wewe, namna alivyogusa maisha yako na namna anavyoweza kuwasaidia wengine
4. Kuwaalika watu waje Kwa Yesu au waje kanisani (Yohana 1:44-50)
Filipo alimwalika Nathanaeli aje Kwa Yesu, Nathanaeli alipokuja Kwa Yesu akamwamini Yesu, Kwa hiyo Sio lazima umwambie mtu maneno mengi hebu Pata nafasi ya kuwakaribisha watu kuja kanisani ili Yesu anayeokoa akutane nao.
5. Kuchangia gharama za uinjilisti (Warumi 10:14-15)
Kuchangia gharama ni pamoja na kuombea harakati za uinjilisti, kuombea washuhudiaji, kuwanunulia vyombo vya uinjilisti washuhudiaji, kuchangia gharama za kuaandaa mikutano ya injili pia kuwasafirisha washuhudiaji au wahubiri.
6. Kuwahubiri watu Kwa njia ya matendo ya kiutu kama vile kuwapa chakula wahitaji, kuwasaidia watu wasiookoka Katika matatizo Yao, kufanya hivyo ni kuitega mioyo Yao ivutwe Kwa Yesu Kwa kuwa Sisi ni wavuvi wa watu.
MAMBO YANAYOSABABISHA UINJILISTI UWE NA NGUVU AU UFANISI
1. Roho Mtakatifu (Matendo ya mitume 1:8)
Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasubiri wajazwe Roho Mtakatifu ndipo waanze ushuhudiaji au waanze kuhubiri injili.
Ijulikane kuwa Kazi ya uinjilisti ni Kazi yenye upinzani mkubwa kuliko Kazi yoyote duniani ndio maana ni muhimu kuifanya ukiwa umejaa Roho Mtakatifu
2. Maombi (Waefeso 6:18-20)
Wahubiri au washuhudiaji wanapaswa kuwa waombaji na kuombewa, maombi huwa yanatengeneza mambo makubwa Katika ulimwengu wa roho, maombi huwa yanavunja upinzania unaowafanya watu wasikubali kuokoka, maombi yanaondoa aibu ya kushuhudia Kwa hiyo ni muhimu kuomba.
3. Miujiza na ishara ( Matendo ya mitume 8:4-8)
Miujiza na ishara Vina nguvu ya kuwavuta watu kumwamini Yesu Kristo ndio maana Yesu huwa anafanya ishara na miujiza ili watu wamwamini kuwa yupo na anaokoa Kwa hiyo ni muhimu kuomba Mungu ajifunue Kwa miujiza na ishara ili watu wapate kuamini.
Ishara ni kitu au jambo linaloonyesha au linalodhihirisha uwepo wa jambo au kitu Fulani au ishara ni udhihirisho wa uwepo au utendaji Kazi wa jambo au kitu Fulani. Kwa mfano ili tujue unaumwa lazima ishara zitajitokeza, ishara ndizo huwa zinaeleza nini kinachoendelea ndani ya mgonjwa. Kwa mfano miti inapoyumbayumba ni ishara ya utendaji au uwepo wa upepo.
Muujiza ni tukio lililotendwa na nguvu zisizo za kibinadamu (supernatural power).
4. Shuhuda (Matendo ya mitume 1:8)
Shahidi anao ushuhuda Kwa hiyo unaposhuhudia usisahau kutoa shuhuda zako binafsi na za watu wengine.
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UINJILISTI
1. Salamu
Unapokwenda kushuhudia lazima uanze na salamu, kama unafanya uinjilisti wa uso Kwa uso au nyumba kwa nyumba usisalimie mtu au watu Kwa salamu ya Imani yako, Kwa mfano usiseme Bwana Yesu asifiwe au tumsifu Yesu Kristo Kwa kuwa ukitumia salamu hizo unaweza usisikilizwe.
(Luka 1:26-28)
Malaika Gabrieli alipopeleka habari njema alianza na salamu Kisha akaeleza ujumbe alikuwa nao.
(Matendo ya mitume 21:40
Mtume Paulo alipopewa nafasi ya kuzungumza alianza na salamu kwanza, aliwapungia watu mkono.
2. Kujitambulisha.
Unapokwenda kushuhudia au kupelekwa habari njema ni muhimu sana kujitambulisha.
(Matendo ya mitume 21:39)
Mtume Paulo alipotaka kushuhudia alianza kujitambulisha, kujitambulisha ni tabia ya Mungu, ukisoma Biblia Mungu alipotaka kusema na watu alijitambulisha kwanza
3. Muombe mtu au watu nafasi ya kuzungumza naye.
Ni muhimu sana kumuomba mtu au watu nafasi ya kuzungumza nao hususani unapofanya uinjilisti wa mtu kwa mtu au wa nyumba kwa nyumba.
(Matendo ya mitume 21:39)
Mtume Paulo baada ya kujitambulisha aliomba nafasi ya kuzungumza, alipopewa nafasi ndipo akaanza kuzungumza.
4. Lugha
Ni muhimu kutumia lugha rahisi ambazo watu watazuelewa, lugha rahisi ni pamoja na mifano, shuhuda na historia.
Hata Yesu alitumia shuhuda, mifano na historia (Mathayo 13:10)
5. Muda
Ni muhimu kuzingatia Muda Katika kushuhudia ili usije ukafanyika kwazo, Kwa mfano kama umemkuta mtu Yuko kazini halafu unataka kuzungumza naye ni muhimu kujali Muda maana Yuko kazini.
6. Mazingira
Ni muhimu kutazama mazingira unayotumia kushuhudia, kama umekutana na mtu njiani msisimae mahali ambapo mtawazuia wengine kupita, kama umekwenda kushuhudia kwenye nyumba za watu Sio vema kuingia ndani Labda ukaribishwe, ni muhimu sana Roho wa Mungu akuongoze Katika kutenda Kazi kulingana na mazingira uliyopo.
(Mathayo 5:1)
Yesu alipowaona makutano alipanda mlimani Kwa kuwa alijua Katika mazingira Yale ni rahisi kusikilizwa akiwa juu, ukiwa juu sauti yako inasikika vizuri na inaweza kwenda mbali ndio maana kwenye mikutano ya injili huwa tunaweka majukwaa Kwa sababu za kijografia.
7. Kuwa na busara kama nyoka na kuwa wapole kama njiwa (Mathayo 10:16)
Nyoka ni mnyama mwerevu na njiwa ni ndege mpole, upole maana yake ni kutotaka makuu au kutotaka migogoro.
Kwa nini uwe mwerevu kama nyoka ni kwa sababu ya usalama wako, kuna wakati Katika kushuhudia au kueleza habari za Yesu unaweza kuinukiwa ikitokea umeanza kuona dalili za kuinukiwa wewe ondoka hapo kwa usalama wako Kwa kuwa Yesu hakututuma kupigana bali kufikisha habari njema.
(Yohana 8:58-59)
Kuna wakati Yesu alikuwa akihibiri ghafla watu wakainuka wakataka kumpiga nawe YESU AKAJIFICHA, hiyo ndio maana mojawapo ya kuwa na busara kama nyoka. Nyoka anapoona hatari huwa anajuficha.
Kwa nini uwe mpole kama njiwa, njiwa huwa hataki makuu hataki migogoro anapoona Kuna hali ya hatari huamua kutulia au kuondoka mahali pa hatari.
Katika kushuhudia Kuna wakati unaweza kukutania na maswali ya kipuuzi, watu kukudharau nakadhalika tena unaweza kudharauliwa na mtu unayemzidi cheo, elimu, uwezo wa kiuchumi nakadhalika inapotokea hali kama hiyo wewe kuwa mpole usitake makuu, usianze kujibu mapigo Kwa kuwa Yesu hakututuma kujibu mapigo bali kupeleka habari njema.
(Mathayo 26:51-53)
Yesu alipokamatwa, Mtume Petro alichomoa upanga akamkata mtu sikio. Yesu Kwa kuwa alikuwa mpole (asiyetaka makuu) alimwambia Petro hata mimi nina uwezo wa kumsihi Baba Mungu aniletee majeshi kumi na mbili ya Malaika wanipiganie lakini huu Sio wakati wake.
Kwa hiyo upole ni wa muhimu sana Katika kushuhudia habari za Yesu maana uinjilisti ni Kazi yenye Vita na maudhi ya kila namna kutoka Kwa shetani LAZIMA UWE MPOLE.
FAIDA ZA UINJILISTI
1. UInjilisti unawafanya watu wamwamini Yesu (Warumi 10:14)
2. UInjilisti unalikuza kanisa kiidadi (Matendo ya mitume 2:40-42)
3. UInjilisti unapunguza wahalifu au waovu Katika jamii.
Wachawi wakiokoka mitaa inakuwa na amani, vibaka, wakora au majambazi wakiokoka watu wanaoishi kwa amani.
(Matendo ya mitume 9:31)
Sauli alipookoka kanisa likaoata raha Kwa kuwa mtesi wa kanisa amebadilika kuwa mhubiri wa injili.
Mungu akubariki
Ni mimi nduguyo
Faraja Gasto - Maarifa Time
+255767955334 (WhatsApp)
+255625775243 (Mawasiliano ya kawaida)
0 Maoni