KUBADILI MATUMIZI YA ARDHI KWA DAMU YA YESU

 


Faraja Gasto

(UFUNUO 5:9-10)

Ardhi inaweza kuyaathiri maisha yako katika namna hasi au chanya (negatively or positively) kutegemeana na namna ardhi ilivyo kiroho.

(Kutoka 20:1-2)

1. Mungu akanena maneno haya yote akasema, 2. Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa”

 

Wana wa Israeeli walianza kupata mateso baada ya utawala mpya kuanza nchini Misri, nchi (ardhi) ya Misri iligeuka kuwa nyumba ya utumwa yaani katika ulimwengu wa roho nchi (ardhi) ya Miari ilibadilika ikawa nyumba ya utumwa.

Ndio maana utaona Mungu alipowatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri aliwaambia amewatoa kwenye nyumba ya utumwa.

N.B Ni muhimu ufahamu ardhi ikoje kiroho (ardhi unayokaa, ardhi unayofanyia biashara, ardhi ya hapo shuleni au chuoni, ardhi ya hapo kanisanin.k) kwa kuwa watu wengi wamejikuta wakipatwa na matatizo mbalimbali kutegemeana na hali ya kiroho ya ardhi.

Kwa mfano katika nchi ya Tanzania kama ardhi imetengwa kwa ajili ya kujenga soko, wewe ukijenga nyumba hapo lazima itabomolewa kwa kuwa umejenga kwenye ardhi ambayo hatakiwi mtu yeyote kujenga makazi, nyumba itabomolewa sio kwa sababu eneo hilo huwezi kujenga nyumba, itabomolewa kwa kuwa matumizi ya eneo hilo ni kwa ajili ya kujenga soko tu.

Ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa roho ardhi huwa inapangiwa matumizi yaani itumike vipi, Mungu anaweza kuitumia kwa matakwa yake na shetani anaweza kuitumiwa kwa matakwa yake, ardhi inaweza kuambiwa cha kufanya na ikatekeleza ilichoambiwa.

(Mwanzo 4:11-12a)

Kaini alipomuua ndugu yake Mungu alimwambia Kaini kuwa atakapolima ardhi “ardhi haitampa mazao”, yaani ni kwamba atakapolima ardhi haitampa ushirikiano. Kwa mantiki hiyo ni kwamba ardhi inaweza kuambiwa cha kufanya na ikafanya.

Damu ya Habili ilipomwagika katika ardhi ilipelekea Kaini akapata shida, jaribu kufikiri ni watu wangapi wanaouawa na damu zao zinamwagika kila siku sehemu mbalimbali, damu hizo huwa zinabadilisha hali ya kiroho ya ardhi husika.

 

(Yoshua 6:26)

Baada ya wana wa Israeli kuuteketeza mji wa Yeriko kwa moto, Yoshua alilaani mtu ambaye atakuja kujenga tena mjia wa Yeriko, kwa hiyo ardhi ya Yeriko ilibeba mauti kwa ajili ya watoto wa mtu ambaye angekuja kujenga mji wa Yeriko.

Ona Yoshua alichosema (Yoshua 6:26)

Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu Yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo”

 

Baada ya muda kupita ona kilichokuja kutokea (1 Wafalme 16:34)

Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni”

 

Huyo mtu aliyeinuka kujenga tena kwenye ardhi ya Yeriko alifiwa na watoto wawili sawasawa na kile alichokisema mtumishi wa Mungu Yoshua.

 

KUBADILISHA MATUMIZI YA ARDHI KWA DAMU YA YESU

 

Ukweli ni kwamba kila aliyemwamini Yesu au kila aliyenunuliwa kwa damu ya Yesu amepewa kumililiki juu ya nchi (Ufunuo 5:9-10) haki hiyo ya kumiliki juu ya nchi inampa mmiliki kuwa na maamuzi ya kufanya mabadiliko ya matumizi ya ardhi ya mahali Fulani.

 

Damu ya Yesu ina nguvu ya kufanya mabadiliko katika ardhi, ardhi inayozaa mapooza inaweza kubadilishiwa matumizi kupitia damu ya Yesu ikawa ardhi inayozaa matunda mazuri.

 

Kila mmiliki kupitia damu ya Yesu anaweza kuamua ardhi itumiwe kwa ajili ya kazi gani, ardhi ikibadilishiwa matumizi katika ulimwengu wa roho na kwenye uliwengu war oho ardhi itatumiwa sawasawa na maelekezo ya ulimwengu wa roho

 

Kama ardhi ina hali ya kiroho ambayo sio nzuri, uliyenunuliwa kwa damu ya Yesu unaweza kuiombea ardhi hiyo ili iwe na hali ya kiroho nzuri.

 

Ushuhuda: Wakati fulani katika eneo fulani nilipokuwa nikiishi niliona watu fulani wanataka kumjengea mungu wao madhabahu, nikomba kwa ajili ya lile eneo ghafla wakasitisha kujenga ile madhabahu pale (mpango ukayeyuka).

 

N.B: Ardhi inaweza ikawa njema kwa watu Fulani lakini kwa watu wengine ikawaathiri, kwa mfano wakati wana wa Israeli walipokuwa Misri, wao waliendelea kuteseka lakini wamisri waliendelea kuishi vizuri.

 

Hitimisho

Unapotaka kufanya mabadiliko ya matumizi ya ardhi anza na toba ili kuondoa uhalali wa shetani kulitumia eneo hilo kwa matumizi ya ufalme wake, baada ya hapo achilia damu ya Yesu juu ya ardhi hiyo ili damu ya Yesu ibadilishe matumizi ya ardhi hiyo katika ulimwengu wa roho (sasa amua unataka ardhi hiyo itumiwe kwa matumizi yapi)

 

Iombee ardhi ya mahali unapofanya biashara, unapofanyia kazi, ardhi ya hapo unapotaka kujenga nyumba, ardhi ya hapo shuleni au chuoni, ardhi ya mahali ambapo watoto wako wanasomea, ardhi ya hapo kanisani n.k

 

Chapisha Maoni

0 Maoni