IFAHAMU HAMASA

 


Kuna kitu kinaitwa hamasa (ari au morali), ni kitu muhimu sana katika kuendeleza au kufanikisha malengo au mipango ya aina yoyote.

Mahali popote kukikosekana hamasa usitarajie kuona mafanikio ya jambo lolote.

Wapo wanafunzi wanafeli kwa sababu ya kukosa hamasa kuhusu masomo, zipo ndoa zinavunjika kwa sababu ya kukosekana hamasa kwa wanandoa, zipo taasisi haziendelei kwa sababu ya kukosekana hamasa, wapo watu wanavunjika mioyo kwa kukosekana kwa hamasa, wapo watu wanahama shule, kanisa, chama n.k kwa kukosa hamasa ya kuendelea kuwepo walipokuwa awali, hayo ni baadhi ya matokeo ya kukosekana kwa hamasa.

HAMASA NI NINI?

1. Hamasa ni nguvu inayomsukuma mtu kujitoa katika kufanya jambo fulani au kuendelea kufanya jambo fulani.

2. Hamasa ni msukumo wa ndani unaomfanya mtu kufanya jambo fulani.

NB: Hamasa inaweza kuongezeka, kupungua na kuisha kabisa pia hamasa inatengenezwa na unaweza kumpatia mtu au watu.

 

 Mbinu za kutengeneza au kumpa mtu hamasa;

1. KUMPA MTU ZAWADI

- Kwa mfano mwanafunzi anapofanya vema kwenye masomo ukimpa zawadi utakuwa umempa hamasa ya kuendelea kufanya vema zaidi.

 

2. KUMPA MTU AHADI KWAMBA AKIFANYA JAMBO FULANI UTAMTENDEA AU UTAMPA KITU FULANI

-Kwa mfano kama mwanafunzi amekuwa anafeli au anafanya vibaya katika masomo, ukimuahidi kuwa akifanya vema utamnunulia simu, computer, begi zuri n.k hiyo ahadi itampa msukumo wa kusoma kwa bidii ili afaulu hatimaye apate hicho ulichomuahidi.

Angalizo: uwe mwaminifu katika kutimiza ahadi kwa kuwa usipotimiza ahadi, hamasa itapungua aau kuisha kabisa.

3. KUTENGENEZA MAZINGIRA WEZESHI

-Kuna watu wanakosa hamasa ya kufanya jambo fulani kwa kuwa hakuna mazingira yanayowawezesha kufanya jambo hilo, sio kama hawana uwezo, uwezo wanao ila hakuna mazingira wezeshi, kuna haja ya kutengeneza mazingira wezeshi ili watu wawe na hamasa ya kufanya jambo fulani.

4. MUONYESHE MTU FAIDA YA HICHO UNACHOTAKA AFANYE

-Kwa mfano Yesu alitaka Petro na wenzake wamfuate lakini Petro akauliza "tumeacha mambo yetu tumekufuata JE! TUTAPATA NINI? Yesu akawajibu kuwa "hapa duniani mtapata mara mia na katika ufalme wa Mungu mtapata uzima wa milele" Yesu aliwaonyesha faida watakayopata wakimfuata.

5. WAONYESHE WATU MATOKEO YA MALENGO AU MIPANGO MLIYOPANGA

-Kwa mfano umewaambia watu wachange pesa wanunue kinanda, hakikisha michango ikikamilika mnunue na uwaonyeshe watu kwa kuwa watu wakiona kazi ya pesa waliyotoa itawapa hamasa ya kuchangia kitu kingine.

6. KUMSHUKURU MTU

-Ukimshukuru mtu kwa kile alichotenda unampa hamasa ya kutenda kingine.

7. KUMUONGEZEA MTU MSHAHARA

-Unapomuongezea mtu mshahara unamtia mtu hamasa ya kufanya kazi zaidi.

Naamini kwa hayo machache umejifunza jambo japo nimekuonyesha faida chache na mbinu chache za kumpa mtu au watu hamasa. Washirikishe wengine.

 

 

Chapisha Maoni

0 Maoni