UWEKEZAJI KATIKA SOKO LA HISA-1

Habarini wana jukwaa, leo nimejiskia kuandika kuhusu soko la hisa kwa hapa Tanzania. Nimeona baadhi ya watu walikua wakiuliza sasa si vibaya hata wakapata kufahamu ni kitu gani hichi. Huu utakuwa ni mwendelezo wa zile mada zangu za uwekezaji kwenye dhamana za serikali (treasury bond + bills) na biashara ya fedha za kigeni. kwa hiyo unaweza kuijumlisha na hii.
Hisa ni nini ?
Kwa lugha rahisi kabisa hisa inawakilisha sehemu ya umiliki katika biashara. Kwa hiyo unapomsikia mtu akisema anamiliki hisa kwenye kampuni fulani, basi ujue ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo kwa asilimia za hisa anazomiliki. Mfano kama kampuni ama biashara ina jumla ya hisa 100 na wewe ukanunua hisa 20 basi wewe ni mmiliki kwa asilimia 20.
Unaponunua hisa pia kuna mtu ambaye anakuwa anaziuza kwa wakati huo huo ndipo wewe ukapata nafasi ya kuzinunua kutoka kwake. Hivo unatakiwa utambue kwamba hisa ni kama bidhaa nyingine zinazouzwa sokoni kama nyanya au vitunguu. Vivo hivyo kama mfano wa nyanya na vitunguu zokoni, kwenye hisa pia kuna wanunuzi na wauzaji ambao wanakutanishwa katika soko ambalo tunaliita soko la hisa.
Soko hili la hisa kama masoko mengine tu ya bidhaa mfano unapokwenda soko la karume utakutana na madalali ambao wao kazi yao inakuwa ni kukushawishi wewe ununue katika duka fulani bila ya wewe moja kwa moja kukutana na mmiliki haswa wa biashara, na biashara ikishafanyika wao kuna kiasi wanakichukua kama ada ya kufanya udalali wa kuuza na pesa nyingine ndiyo inakwenda kwa mmiliki wa biashara. Vivo hivyo katika masoko ya hisa utakutana na madalali kama hawa ambao tunawaita brokers. Pindi unapotaka kununua au kuuza hisa lazima upitie kwao kwanza kwa sababu katika hisa, wao ndio haswa wana uhalali wa kisheria kushiriki moja kwa moja katika soko la hisa.
Soko la hisa kwa Tanzania
Tanzania pia kama nchi nyingi za ulimwengu wa kileo nasi tuna soko letu la hisa ambalo ni Dar es salaam stock exchange DSE kwa wasio fahamu DSE ipo jengo la Golden Jubilee Tower floor 10. Soko letu la hisa ambalo naweza kusema ni changa ukilinganisha na masoko ya nchi nyingine lina takribani makampuni 21.
Kama nilivooleza awali kwa Tanzania ukitaka kununua au kuuza hisa zilizo orodheshwa na DSE utatakiwa kwanza upitie kwa brokers ambao huwa wanakuwa na taarifa kamili za bei zilizopo sokoni kwa wakati huo na mabroker wengi wanatoa huduma ya ushauru kuhusu kufanya maamuzi ya kununua au kuuza maana ni watu wenye uelewa mkubwa kuhusu masuala ya hisa. Kwa Tanzania tuna mabroker kama Orbit Securities Co. Ltd, Rasilimali Limited, Solomoni Securities Ltd, Core securities Ltd, Tanzania securities Ltd, Vertex International Securities japo pia kuna bank zina act kwa niaba ya mabroker fulani mfano CRDB Bank kwa hiyo ina maana hapo banki pia unaweza kuweka order ya kununua au kuuza hisa.
Kingine muhimu kabla ya kuuza au kununua hisa lazima uwe na account ya banki ambayo malipo mengi yatapitia huko pale unapouza au pindi ukipata gawio lako la hisa kutokana na faida ya kampuni.

Umuhimu wa kuwekeza kwenye hisa
Mwekezaji katika hisa anaweza kufaidika kwenye mambo yafuatayo yanayotokana na umiliki wake wa hisa.
i) Gawio la hisa (dividend) kwa sababu tumeshaeleza hapo juu kwamba ukimiliki hisa unahesabika wewe ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hivo basi pale kampuni inapopata faida kuna gawio ambalo utapata kulingana na idadi ya hisa unazomiliki. Mfano kwa mwaka kama huu banki ya CRDB ilitangaza gawio la sh. 15 kwa kila hisa moja. Lakini hapa kwenye gawio sio lazima kupata kila mwaka kutegemeana na sera za kampuni. Kama kampuni haipati faida ama ipo kwenye kujitanua ina maana faida itayopatikana itawekwa kwenye kupanua kampuni.
ii) Kupanda kwa bei ya hisa kunatoa fursa ya kuongeza utajiri wako kama ukiamua kuuza. Hapa naongelea personal portfolio ya mtu binafsi kukua kama itatokea bei ya hisa itapanda. Mfano mzuri kwa wale walionunua hisa za NMB mwaka 2009 kwa shilingi 600 na leo hii hisa ya NMB ni 2900 kwa hiyo unaona kuna ongezeko kama la 2300 kwa kila hisa uliyonunua 2009. Ikiwa na maana kama ungeweka 12,000,000 ungenunua hisa 20,000 ambazo kwa leo hii kama ungeziuza ungekuwa na kitu kama 58,000,000. Sasa can you imagine after seven years ile milioni 12 inakupa pesa ya kununua apartment ya NHC sio faida hiyo?
iii) Zaweza kutumika kama dhamana ya kuombea mkopo katika taasisi zinazotoa mikopo. Hapa tunaongelea kitu kinachoitwa stock-secured loans. Kwa taasisi za fadha wanaweza kutupa muongozo namna ya kutumia hisa zako ili ziwe dhamana ya mkopo. Lakini kitu kikubwa kabisa ni kwamba sio kila hisa yaweza kutumika kama dhamana. Kinachoangaliwa hapa ni liquidity ya hisa nikiwa na maana zile hisa ambazo zinauwezekano wa kuuzika kwa haraka na zenye bei iliyo stable ndizo hasa taasisi za fedha wanazipa kipaumbele kwa sababu zinakuwa na hatari kidogo. Kwa Tanzania hapa naweza kusema hisa kama za TBL, TWIGA CEMENT, CRDB, TCC, NMB na SWISSPORT naweza kusema zipo more liquid na unaweza kutumia kama dhamana bila usumbufu wowote.
iv) Zinahamishika, ikimaanisha zinaweza kuwa kama urithi kwa watoto wako. Kwa nchi za magharibi ambazo masoko yake ya hisa yamekuwapo kwa zaidi ya karne moja. Kuna hisa ambazo mpaka sasa zinamilikiwa na watu lakini zilinunuliwa miaka mingi iliyopita na mababu zao. Utaongelea makampuni kama J.P Morgan, General Electric, Ford, GM nk ambazo umiliki wa hisa umetembea vizazi na vizazi.

Who is who in stock investing?
Nimeandika kwa kiingereza kuweka msisitizo. Nikiwa na maana kwamba nataka kuonesha nguvu ya kuwekeza katika soko la hisa inaweza kukufanya uwe mtu wa namna gani katika ulimwengu wa sasa.
Uwekezaji katika hisa umetengeneza matajiri wakubwa katika ulimwengu wa sasa. Watu kama kina Warren Buffet, Carl Icanh, George Soros na wengineo wengi. Hao niliowataja hawakugundua chochote kwenye maisha yao kama mabilionea akina Bill Gates, Larry Elison, Steve Jobs, Henry Ford na wengineo wengi. Ila utajiri wao haswa ulitokana na kuwekeza kwenye hisa.

Mtu kama Warren Buffet na Carl Icanh leo hii wanamiliki makampuni mengi ambayo hawakuyaanzisha wenyewe bali wameyamiliki kwa kununua hisa mpaka wakawa major shareholders.
Hata kwa nchi kama Tanzania huwezi kuamini kuna watu wametengeneza utajiri wa ajabu kwa hisa hizi hizi unazoziona pale DSE. Binafsi nilibahatika kukutana na mtu akaniambia yeye alinza kuwekeza kwenye hisa mwaka 1999 na mpaka wakati ananisimulia ananiambia alikua na portfolio ya karibu milioni 500. Sasa hapo unaweza kufikiri mwenyewe how fast kuwekeza kwenye hisa kunaweza kukufanya kwa kiasi fulani na wewe ukaonekana na wewe ni mtu fulani.
Lakini dont be carried away easily kama kawaida kutengeneza utajiri kunahitaji akili. Sio tu kwa sababu unapesa basi unaenda na wewe kununua hisa. Kuna vitu vingi sana vya kuangalia kabla ya kwenda kununua hisa. Huu ni uwekezaji kama uwekezaji mngine ambao unakuwa na hatari (risks). Saa nyingine unaweza kwenda kununua hisa lakini kumbe kampuni inaenda kufa siku za mbeleni. Au pia kampuni haioneshi mwelekeo wowote wa kufanya vizuri siku za mbeleni. Kwa hiyo inamaana hapo kwa lugha ya kihuni utakua umeingia choo cha kike hahahahahahah. Maana kama kampuni hai perform, haitengenezi faida ina maana 1) bei ya hisa itashuka halafu 2) hisa zitakua haziuziki tena kwa hiyo hamna namna yoyote ya kurudisha pesa ulizowekeza. Mfano tu hapa Tanzania kuna kampuni kama Precision Air ambalo halijawahi kutoa dividend kwa shareholders na hisa zake pale DSE haziuziki maana hazihitajiki kwa sababu kampuni hai perform.
Ushauri kutoka kwa Buffet.
Ili uweze kufanikiwa katika uwekezaji wako wa hisa na huko mbeleni uweze kuchekelea utajiri ulioukusanya kama yule rafiki yangu wa milioni 500, ni budi kujua unawekeza kwenye hisa za makampuni yapi.
Kujua mbinu murua za kuwekeza kwenye hisa ntaleta mezani na kujadili kiufupi njia ambazo aliziainisha bilionea Warren Buffet ambaye kama nilivooleza hapo juu ni moja ya mwekezaji wa hisa kuwahi kutokea mpaka sasa kwenye dunia hii.
Ntajaribu kuweka baadhi tu ya njia au mambo makubwa ya kuangalia kabla ya kufikia maamuzi ya kuwekeza kwenye hisa. Katika njia hizo Buffet aliziorodhesha katika makundi manne ambayo ni 1) viashiria vya biashara yenyewe (business tenets) 2) menejimenti ya kampuni husika (management tenets) 3) viashiria vya kifedha (financial tenets) 4) viashiria vya soko kwa kampuni husika (market tenets).
Buffet anashauri kwamba ukishajiridhisha na utafiti wako kwenye kampuni fulani dhidi ya viashiria kwenye makundi hayo manne basi ndio wasaa mzuri wa kufanya uwekezaji kwenye hisa zake na baadae uje na wewe uchekelee.
Katika viashirio hivo kuna maswali mwekezaji unatakiwa ujiulize kama

- Je biashara au kampuni nnayotaka kuwekeza inaeleweka ?
- Je biashara au kampuni ina historia gani ya uendeshaji wake (operating history)?
- Je biashara au kampuni ina future yoyote nzuri kwa kipindi cha mda mrefu ujao (favourable long term prospects)?
- Je menejimenti ya kampuni au biashara ina ufanisi wa kufanya maamuzi?
- Je menejimenti ya kampuni ina uhusiano mzuri na kuaminika na shareholders?
- Je kampuni inapata faida?
- Je gawio la hisa la kampuni linaleta maana?
- Je thamani halisi ya biashara ni ipi ?

Ikiwa utajiridhisha na maswali hayo hapo juu kwa kiwango cha at least cha asilimia 70 za kuridhika basi nenda kanunue hisa. La umeridhika kwa asilimia 30 halafu wewe unaenda kununua, hapo hutakua tofauti na mtu anayecheza kamari kudhani kwamba mambo mbeleni yatakuwa mazuri akati viashiria havioneshi hivo.
Nimeliona sana hili tatizo kwa Tanzania hapa, mtu akishasikia IPO basi yeye ana rush tu kwenda kununua bila hata kupima angalau viashiria vichache hapo juu. Kwa nchi za wenzetu biashara hii inachukuliwa kwa umakini mkubwa sana na hata wengine kabla ya kununua wana seek advice kwa wataalamu wa masoko ya hisa.
Na ndio maana leo hii tunawashuhudia watu kama kina Warren Buffet, kama ingekuwa hawana umakini wowote wa kuwazua kabla ya kufanya maamuzi ya kuwekeza wasingekuwa hapo walipo.
Kwa hiyo ndio hivyo, sio wote wana akili kama za Buffet ila pia haikuzuii kutumia akili yako kufanya uchanganuzi wa kuwekeza kwenye hisa na baadae ije kukulipa. Maana ieleweke kwamba unachokiwekeza ni pesa zako kwa hiyo sio vema kufanya maamuzi ya kupoteza pesa bila kuwa na uhakika angalau kwa asilimia fulani.
Mwisho kabisa kwa sababu hii ni elimu pana na hapa nimetoa tu kamwanga ningependa kusikia kutoka kwenu pia wana jukwaa maana naamini kuna watu wanajua mambo mengi mnoo kwenye hii field. Cc Bavaria
Asanteni sana, nawatakia uwekezaji mwema.


Nyongeza kutoka kwa Mwl.Faraja Gasto
Kabla ya kuwekeza ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa Mungu maana ndiye anayefahamu yaliyopita, yaliyopo na yajayo.


Chapisha Maoni

0 Maoni