Mwl. C. Mwakasege
(1)Omba toba ili Mungu akusamehe! Ndiyo - omba toba ili Mungu akusamehe kwa kushindwa kuomba! Swali unaloweza kuuliza, ni kutaka kujua ikiwa kutokumwomba Mungu ni dhambi!
Nabii Samweli kuna wakati aliongea na watu wake, akasema: "Walakini mimi, hasha! nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi;......"(1Samweli 12:23). Iwe ni kutokuwaombea wengine au *kutokujiombea wewe - kutokuomba ni dhambi!*
Kutokumwomba Mungu *si udhaifu bali ni dhambi!* Udhaifu katika maombi ni kule kutokujua jinsi ipasavyo! Ndiyo maana imeandikwa: " kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba ipasavyo........"(Warumi 8:26)
Kufuatana na 1Yohana 3:4 dhambi ni uasi au ni kwenda kinyume cha maelekezo ya Mungu. Kuomba ni agizo na mwaliko kutoka kwa Mungu, ili upate kuongea naye. Kutokumwomba ni kukataa mwaliko huo; na ni sawa na kukataa kutii agizo la Mungu. Kwa hiyo kutubu ili usamehewe kwa kutokumwomba ni hatua sasa. Mungu atakusamehe, na kurudisha ndani yako hamu ya kuomba.
Mungu akusaidie kama hili ni tatizo kwako.
(2) Ondoa hali ya *kujihukumu moyoni mwako*! Kujihukumu moyoni mwako kunakuondolea ujasiri wa kwenda mbele za Mungu na kuomba.
Biblia inasema hivi: "Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, twalipokea kwake...."(1Yohana 3:21,22). Huu ni mstari unamhusu yule anayeshindwa kuomba, au kwa sababu anadhani ya kuwa hata baada ya kutubu Mungu hajamsamehe! Au ameshindwa kujisamehe kwa sababu ya kosa alilomkosea Mungu, hata kama amelitubia kosa hilo! Au anajisikia vibaya moyoni, akidhani ya kuwa, kwa kuwa wale wanaomzunguka hawaonyeshi hali ya kumsamehe kwa kosa alilofanya, basi anafikiri na Mungu naye hajamsamehe hata kama ametubu!
Amini ya kuwa Mungu hasemi uongo! Ukitubu dhambi zako huwa anakusamehe na kuifuta dhambi hiyo! Hii ni sawa na Isaya 1:18 na Isaya 43:25 na 1Yohana 1:9. Mungu anasema hivi kwako:" *Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie maana nimekukomboa"(Isaya 44:22)
(3)Funga katika nafsi yako"! Hebu soma mstari huu: "Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; maombi yangu yakarejea kifuani mwangu"(Zaburi 35:13).
Daudi aliyasema hayo alipokuwa anatafuta utatuzi wa yeye kushindwa kuomba kama alivyokuwa anaomba huko nyuma! Daudi anasema kufunga katika nafsi yake, kulisaidia kurejesha tena maombi kifuani mwake! Na wewe wewe unaweza ukatumia mbinu kama hii, ili kurudisha tena uwezo wako wa kuomba!
Fahamu ya kuwa: *kuna tofauti kati ya kufunga katika mwili, na kule kufunga katika nafsi*. Kufunga katika mwili maana yake, kuunyima mwili mahitaji yake muhimu kama chakula; na maji na usingizi. *Kufunga katika nafsi maana yake,kuinyima nafsi yako mahitaji yake muhimu yanayopatikana kwa njia ya macho na masikio*. Lakini ikiwa ni kufunga katika mwili au ni katika nafsi; ni muhimu uongozwe na Roho Mtakatifu sawasawa na neno la biblia.
Kwa hiyo, kufunga katika nafsi kunatokea mtu anapofanya maamuzi ya makusudi kwa msukumo wa Roho Mtakatifu moyoni mwake, ili kujitenga na kukaa kwa utulivu mahali ambapo hakuna usumbufu juu ya macho yake na masikio yake. Ukifanya hivi, tarajia maombi kurudi kifuani mwako sawa na Zaburi 35:15.
Tunakuombea ili Mungu azidi kukufundisha na kukuongoza katika kufanya maombi ya kufunga yenye faida.
(4)Fanya maamuzi thabiti moyoni mwako *kuwa utakuwa mwombaji!”*
Fahamu hili ya kuwa: Kufanya maombi ni maamuzi kwanza, kabla hakijawa kitendo!
Kufanya maombi ni jambo la moyoni kwanza, kabla halijawa jambo la mdomoni! Ikiwa huna maamuzi thabiti moyoni mwako ya kuwa mwombaji, ina maana na kuomba kwako kutakuwa kwa matatizo.
Mungu anasema katika kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati 7:14 ya kuwa: “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao”. Neno hili *“ikiwa”* linatuonyesha ya kwamba Mungu anataka tujue ya kuwa: Kuomba au kutokuomba ni hiari na maamuzi ya mtu!
Tunakuombea Mungu akusaidie, ili maamuzi yako ya kuomba yawe thabiti, na yasiyumbe – yumbe; ili uweze kuwa mwombaji, kwa kadri ya Roho wake atakavyokuwa anakuongoza!
(5) Je, unasikia kusita moyoni mwako kila unapotaka kuomba? Lakini pia, inawezekana husikii kusita kuomba mambo yote, ila kuna mambo fulani – fulani tu ambayo unasikia kusita moyoni mwako kuyaombea.
Ukitaka kulishinda tatizo hili la kusita kuomba, ambalo linakufanya unashindwa kuomba; basi, tafuta ufumbuzi wa hali hiyo ya kusita kuomba! Na baada ya hapo naamini utaweza kuomba! Maisha ya Ibrahimu yanatupa jibu tunaposoma jambo alilofanya akisubiri kumpata mtoto wake Isaka.
Biblia inasema: “Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa Imani, akimtukuza Mungu; huku akijua ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi”. (Warumi 4:20,21).
*Kumbuka*: Kusita kuomba kunatokana na hali ya kutokuamini moyoni mwa mtu anayetaka kuomba.
Ukishinda tatizo la kutokuamini, utashinda pia na tatizo la kusita kuomba! Na tatizo la kutokuamini unalishinda kwa kulitafakari neno la biblia lililo na ahadi ya Mungu juu ya lile unalotaka kuliombea!
Tafakari hilo neno hadi ahadi hiyo igeuke picha na uione moyoni mwako! Kutokuamini ni matokeo ya kutokuwa na uhakika kama Mungu atakupa au hakupi hilo unaloliomba kwake! Hii ni kufuatana na Waebrani 11:1 na Warumi 10:17.
(6)Je, umepita au unapita kwenye taabu maishani mwako, kiasi kwamba huwezi kuomba, kwa *sababu nafsi yako imakataa kufarijika?*
Daudi aliwahi kukumbana na tatizo kama hili maana anatuambia hivi: “Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana, mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea, nafsi yangu ilikataa kufarijika. Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika, nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.
Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike, naliona mashaka nisiweze kunena” (Zaburi 77:2-4). Ni wazi kwamba taabu alizokuwa anapitia Daudi, ziliumiza nafsi yake, na nafsi yake ikakataa kufarijika, na mwisho wake alishindwa kuomba!
Je, unapita katika hali kama hii? Fanya kama alivyofanya Daudi katika kutatua tatizo lake hilo; na wewe utatatua tatizo kama hili ikiwa unalo! Daudi alifanyaje? Daudi alikuwa anafanya mambo mawili makubwa kila akikumbwa na hali kama hii:
👉 1. Alitafakari matendo makuu ya Mungu aliyowahi kufanyiwa au aliyowahi kusikia Mungu kayafanya;
👉2. Aliisemesha nafsi yake juu ya matendo makuu ya Mungu na juu ya ahadi za Mungu! Soma Zaburi 77:10 – 12 na Zaburi 42:5,6.
Kwa kuwa taabu zinaweza zikaifanya nafsi ipoteze Imani yake kwa Mungu; basi, chukua hatua ya kuilazimisha nafsi yako kutafakari matendo makuu ya Mungu na ahadi zake! Mwanzoni inaweza ikawa ngumu kwa nafsi kufarijika, lakini ukiendelea hivyo kwa siku kadhaa, naamini nafsi itafarijika, na wewe utapata uhuru wa kuomba uliokuwa umeupoteza!
*Kumbuka*: Neno la Mungu linauwezo wa kuiponya nafsi iliyoumizwa.
Tunakuombea ili Bwana Yesu aendelee kukutunza!.
1 Maoni
Somo hili limenipa hatua nyingine ya kiwango cha maisha yangu ya Kiroho. MUNGU aendelee kukuzidisha na kukuinua. Ameni nimebarikiwa sana
JibuFuta