UMUHIMU WA KUOMBEA MIFUMO YA NCHI



Kila nchi huwa ina mifumo yake kutegemeana na sheria na ukanda ilipo nchi husika na kila mfumo huwa unasimamiwa na chombo fulani kilichopewa mamlaka ya kisheria kuusimamia mfumo huo ili ufanye kazi kulingana na matakwa ya nchi husika kutokana na malengo waliyojiwekea.
Wakristo hatutakiwi kubaki tukiomba tu, bali inatakiwa ifike hatua wakristo waingie kwenye mifumo ya nchi ili kuibadilisha ambayo haijakaa vizuri, unaposoma habari za wayahudi waliokuepo pale kwenye ufalme wa Ahasuero, walipotangaziwa kuuawa walimwomba Mungu huku baadhi yao wakiwa ndani ya mfumo; Esta alikuwa Malkia na Mordekai alikuwa akifanya kazi ya ulinzi katika ikulu ya Mfalme Ahasuero, kutokana na uwepo wao kwenye mfumo katika ule ufalme uliwasaidia kujua nini kinachoendela ambacho kina madhara kwao na walipojua ndipo walipokwenda mbele za Mungu kuomba(Esta 4:17)
Kosa ambalo tunalifanya sisi kama kanisa la Mungu, tunaomba huku hatuko tayari kuingia kwenye mifumo ya nchi na ndio maana kuna mambo yanatokea ghafla na inatupa wakati mgumu kuomba.
Mfumo una nguvu kubwa ya kimaamuzi juu ya maisha ya watu wa nchi husika, mfumo unaweza kuamua watu wawe katika hali gani kiroho na kimwili haijalishi wanaitaka hali hiyo au hawaitaki.
Mfumo unaweza kuharibu maono au ndoto za watu kama watu hawatakuwa makini katika suala la maombi kwa kuwa shetani huwa ana tabia ya kuutumia mfumo kuua huduma au karama za watu, kuua maono au ndoto za watu na pia kutengeneza hali za kiroho zitakazoleta madhara katika maisha ya watu.
Katika hili nitajikita zaidi kuzungumzia mifumo sita kama ilivyooneshwa hapa chini ili uweze kuona jinsi mifumo ilivyo na nguvu ya kimaamuzi juu ya maisha ya watu kiroho na kimwili.

1.     Mfumo Wa Elimu Wa Nchi
2.     Mfumo Wa Siasa Wa Nchi
3.     Mfumo Wa Sheria Wa Nchi
4.     Mfumo Wa Uchumi Wa Nchi
5.     Mfumo Wa Kupata Mamlaka Au Nafasi Ya Uongozi
6.     Mfumo Wa Maamuzi Wa Nchi

MFUMO WA ELIMU WA NCHI
Katika nchi nyingi za bara la Afrika kumekuwa na wimbi kubwa la vijana ambao wakimaliza masomo yao hususani kuanzia ngazi ya kidato cha nne, sita na vyuo wanakuwa hawana uwezo wa kuendesha maisha yao kwa sababu mfumo wa elimu haukuwaandaa kujitegemea baada ya kuhitimu masomo yao, hivyo basi vijana wengi wamekuwa tegemezi kwa wazazi huku wakiinyooshea vidole serikali kwa kuwa hakuna ajira za kuwatosheleza vijana wote wanaomaliza masomo yao.
(Danieli 1:1-5)
Ukisoma andiko hilo utaona palitokea uhitaji katika eneo hilo la Babeli kwa kuwa Mfalme wa Babeli alihitaji watu watakaosimama mbele ya Mfalme lakini ulitengenezwa mfumo wa upatikanaji wa watu hao, utaratibu wa kuwapata watu hao ulikuja kwa njia ya mfumo wa elimu, mfumo uliwahitaji vijana ambao watafundishwa elimu ya wakaldayo na lugha yao na baada ya kuhitimu masomo yao ndipo wapate nafasi ya kusimama mbele ya Mfalme.
Mfumo wa elimu ndio uliamua ni nani wa kusimama mbele ya Mfalme, mfumo ule uligusa hadi masuala ya kiroho ndio maana baada ya wale vijana kuanza masomo ghafla wanapata ofa ya kupata chakula bure lakini chakula kile kilikuwa kimeunganishwa kwa miungu ya Babeli, kutokana na hilo vijana wa kiisraeli walikataa kula kile chakula lakini wakiwa wako kwenye mfumo wa elimu uliokuja na vyakula vilivyounganishwa kwa miungu ya Babeli.
Ninachotaka uone kwenye Biblia ni jinsi ambavyo mfumo unaweza kutumiwa na shetani kuwakamata watu wawe chini ya mamlaka yake. Mfumo wa elimu wa Babeli wa wakati huo ulikuwa unawaandaa watu ambao watakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwenye ikulu ya Mfalme wa Babeli.
Kufikia hapo nataka nikuulize swali je! unaujua mfumo wa elimu wa nchi yako? Je! mfumo wa elimu wan chi yako unawaandaa watu kuwa watu wa aina gani baada ya elimu? Je! mfumo wa elimu wan chi yako unajua una mchango gani wa kiroho kwenye maisha ya watu?  

MFUMO WA SIASA WA NCHI
Rejea maana ya siasa katika sura ya kwanza, mfumo wa siasa umegawanyika katika makundi makuu mawili (i)mfumo wa chama kimoja(single party system)  (ii)mfumo wa vyama vingi(multi-party system). Mfumo wa siasa ambao umechukua sehemu kubwa ni mfumo wa vyama vingi(multi-party system) mfumo huu ndio unaruhusu ushindani(political competition) na ushindani huo ndio ambao huzalisha kampeni na kampeni ambazo zimekuwa  zikifanyika kwa misingi ya kudhalilishana, kutishiana, kutukanana n.k na ndio maana nyakati za kampeni kumekuwa kukitokea machafuko mengi.
Je! mfumo wa vyama vingi ni mbaya? Kwa mtazamo wangu ninaweza kusema mfumo huu sio mzuri kwa kuwa umejengwa juu ya misingi ya ambayo haikubaliki kibiblia kwa kuwa Mungu anatawala kifalme na ndio maana Yesu alifundisha ufalme wako uje (Mathayo 6:9-10) hata Bwana Yesu anaitwa Mfalme wa wafalme na Bwana wa Mabwana (Ufunuo 19:16).
Siasa ya kwenye mfumo wa kifalme hakuna kitu kinachoitwa vyama vingi (multi-partism) bali mfalme anarithishwa kiti cha ufalme bila kuchaguliwa na watu lakini kwenye mfumo wa siasa wa vyama vingi kiongozi au viongozi wanapatikana kwa njia ya uchaguzi(election) baada ya muda Fulani.
SWALI: Kwa kuwa misingi imekwisha haribika tufanye nini?
Nizidi kutoa mfano kwenye mifumo tuliyonayo hapa katika bara la Afrika, imekuwa ikisikika kuwa “siasa ni uongo” lakini je! kweli siasa ni uongo? Jibu ni kwamba siasa sio uongo ila uongo wanao baadhi ya wanasiasa, kinachosababisha siasa ionekane kuwa uongo ni mfumo wa siasa wa nchi ndio unaopelekea wanasiasa wawe wa kweli au waongo, kiuhalisia mfumo wa siasa wa nchi nyingi za Afrika unatengeneza wanasiasa wasio wakweli ndio maana wanasiasa wengi wa Afrika wamekuwa wakiahidi mambo ya uongo ili wapate kura nyingi katika chaguzi mbalimbali, nakumbuka siku moja nilikuwa nasikiliza redio Fulani na palikuwa na mdahalo unaozungumzia kipi ni muhimu kati ya afya za watu kwanza au uchumi kwanza, katika mdahalo huo alihojiwa mbunge wa jimbo Fulani Yule mbunge alisema wakati akiwa kwenye kampeni za kugombea ubunge alikuwa akiwaambia watu kuwa endapo atapata hiyo nafasi atapambana ili kukomesha biashara ya tumbaku kwa kuwa tumbaku ina madhara makubwa kwenye afya za watu lakini mbunge huyo alisema kuwa punde si punde watu walimjia juu wakamwambia usipoachana na huo mtazamo wako hautapata kura kwa hiyo ilibidi aachane na hilo suala la kukomesha biashara ya tumbaku, kinachosababisha watu wasitake siasa zenye ukweli ni MFUMO WA SIASA WA NCHI na hapa ndipo wanasiasa huonekana kuwa watu wenye ahadi za uongo ila shida sio wanasiasa shida ni MFUMO na kutokana na mfumo huu umewazuia wakristo wengi kujiingiza kwenye siasa kwa madai mbalimbali ikiwemo na mtazamo huu kuwa siasa ni uongo, lakini ni vema wakristo waelewe kuwa ikiwa mfumo umeshaharibika, lazima watu wanaomjua Mungu waingie huko ndani ya mfumo ili kuubadilisha, wakina Danieli walipoona kuna ajenda ya miungu kwenye vyakula vilivyokuja kupitia mfumo wa elimu walikataa kula kile chakula lakini hawakuacha masomo, waliendelea na masomo yao lakini walikataa kula chakula kilichokuja kupitia mfumo wa elimu. Wakristo wanaweza kuingia kwenye mfumo wa siasa lakini wakaepuka kujiingiza kwenye mambo yasiyompendeza Mungu katika mfumo wa siasa kuliko kuwaachia watu wasiomjua Mungu watawale mfumo wa siasa.
Waliosababisha mabadiliko ya mifumo pale Babeli walikuwa watumishi wa Mungu waliosimama kwa imani juu ya Mungu wao na wakabadilisha mifumo mbalimbali pale Babeli, kama wakristo wataendelea kuogopa kuingia kwenye mifumo iliyoharibika ili waibadilishe basi tutarajie kuona shetani akitawala mifumo mbalimbali katika nchi na kama shetani atakamata mifumo mbalimbali katika nchi ni vema kila mtu aelewe hili lilionenwa na Biblia  “mwenye dhambi akitawala watu huugua bali wenye haki watawalapo watu hufurahi”

MFUMO WA SHERIA WA NCHI
Mfumo wa sheria wa nchi ndio ambao huwa unapanga taratibu, kanuni za kufanya mambo mbalimbali katika nchi na aina za adhabu kulingana na makosa yaliyofanyika, mfumo wa sheria kama hautaombewa unaweza kutumiwa na shetani kuzuia kazi ya Mungu katika nchi, kuwaharibu watumishi wa Mungu katika nchi, kuondoa uhuru wa kufanya mambo mbalimbali ya msingi n.k.
Utaratibu wa kutunga sheria hususani kwa nchi zinazotawaliwa kwa mfumo wa kidemokrasia, sheria zinatungwa na Bunge na baada ya kutungwa na Bunge inakuwa kama muswada(bill) na baada ya hapo muswada unapelekwa kwa raisi wa nchi ili itiwe muhuri na ikiisha tiwa muhuri ndipo sheria inakuwa halali kutumika.
Nitoe mfano kwa nchi ya Tanzania, katika nchi ya katiba ya nchi ambayo ndio sheria mama ya nchi imeainisha uhuru alionao kila mtanzania kwa mfano katika ibara ya 18 imeruhusu mtu kuwa na uhuru wa kutoa maoni. Ibara ya 19 ya katiba ya nchi ya Tanzania imempa mtu uhuru wa kuamini dini atakayo. Kwa hiyo uhuru huo mtu anaupata kwa sababu sharia ndio imempa huo uhuru .
(Danieli 6:4-17)
Danieli alitupwa kwenye tundu la simba kwa kuwa sheria zilizingatiwa hatimaye akatupwa kwenye tundu la simba japo hakuwa na hatia ila ilikuwa ni ajenda iliyotengenezwa na watu waliokuwa kinyume na yeye.
Kwa hiyo suala la kuomba linatakiwa lianze kabla sheria hai/hazijatungwa na kama zimekwisha tungwa ni muhimu tuombe kwa ajili ya watu wanaosiamamia utekelezaji wa sheria hizo.

MFUMO WA UCHUMI WA NCHI
Nianze kwa kukuuliza swali hili. Je! katika nchi yako watu matajiri au wau waliofanikiwa katika nchi wanamwabudu Mungu aliye hai kupitia Yesu Kristo au wanaabudu miungu?
Ukiona katika nchi yoyote watu wanaomwabudu Mungu wa kweli kupitia Yesu Kristo hali zao za uchumi sio nzuri ni vema ujue sababu mojawapo ni mfumo wa uchumi wa nchi husika hautawaliwi na Mungu aliyeziumba mbingu nan chi kwa hiyo endapo katika nchi hiyo mtu atahitaji kutajirikia lazima ajiunganishe na huyo mungu anayetawala mfumo wa uchumi wa nchi la sivyo lazima awe na maarifa ya kiMungu yatakayomsaidia yeye kufanikiwa katika nchi ambayo mfumo wake wa uchumi unatawaliwa na miungu.
 Jaribu kutazama nchi nyingi za Afrika na nchi zingine duniani, mafanikio ya watu wanaomwabudu Mungu wa kweli ni kidogo ukilinganisha na watu wanaoabudu  miungu na hata kama ikitokea mtu amefanikiwa anakuwa amepitia ugumu wa kutosha kwa sababu mfumo wa uchumi wan chi haujatawaliwa na Mungu, na hapa ndipo utaelewa maana ya Yesu kuwafundisha wanafunzi wake waombe kuwa “ufalme wa Mungu uje” ili mapenzi ya Mungu yatimizwe na kile ambacho anakitaka Mungu kitimie kwa kuwa mapenzi ya Mungu yanapotimizwa ndipo inakuwa rahisi kwa watu wa Mungu kupata mkate wao wa kila siku (Mathayo 6:9-10).
Ni muhimu kuomba mapenzi ya Mungu yatimizwe katika kila mfumo wa nchi kwa kuwa mapenzi ya Mungu yanapotimizwa ndipo wenye haki wanaweza kusitawi lakini ikiwa mfumo wa uchumi wan chi utandelea kutawaliwa na miungu basi tutaraje kuona wafanyabiashara wakubwa katika nchi wakiwa waabudu mashetani(watoa makafara kwa mashetani).

MFUMO WA KUPATA MAMLAKA AU NAFASI YA UONGOZI
Suala la upatikanaji wa nafasi ya uongozi au mamlaka katika nchi hutegemeana na sheria za nchi au mfumo unaotawala katika nchi.
Mfumo wa upatikanaji wa nafasi za uongozi au mamlaka katika nchi nyingi hutegemea siasa, wanasiasa ndio ambao wana nafasi nyeti za kiuongozi na wao ndio huchagua viongozi wengine wa nafasi tofautitofauti, mfumo huu lazima utawaliwe na Mungu kwa kuwa kama ataingia kwenye nafasi mtu wa chama Fulani cha kisiasa lazima kuna watu atawapa nafasi za kiuongozi au mamlaka kwa misingi ya urafiki, itikadi ya chama chake au kulipa fadhila. Kumbuka “wakitawala waovu watu huugua bali wakitawala wenye haki watu hufurahi’ 

MFUMO WA MAAMUZI WA NCHI
Mfumo wa maamuzi wa nchi hutegemeana na nchi husika kwa nchi nyingi duniani maamuzi mbalimbali hufanyika kwatika Bunge na mahakama na kama shetani atatawala huu mfumo wa maamuzi katika nchi ni wazi kuwa yatasikika maswali na vilio kama Nabii Habakuki alivyosema  (Habakuki 1:12-17)
Ikiwa Bunge litakaliwa na watu wasiomwabudu Mungu aliyeziumba mbingu na nchi basi ni wazi yatapitishwa mambo maovu kama vile; ndoa za jinsia moja zitaruhusiwa, kutoa mimba itakuwa ruksa n.k kwa kuwa mfumo wa maamuzi umeingiliwa na adui shetani.

Chapisha Maoni

0 Maoni