UMUHIMU WA KUOMBEA SAFARI ZA VIONGOZI WA NCHI NA SAFARI ZA WATU WANAOINGIA NA KUTOKA KATIKA TAIFA




Mwaka 2016 tumeshuhudia Raisi wa Marekani Donald Trump akibadilisha kabisa hali baada ya kutangaza hataki wageni katika taifa la Marekani, ninachozungumzia mimi sisemi wageni wasiingie katika taifa Bali ninachosema ni kwamba ni muhimu kuombea ujio wa wageni waingiao kwenye taifa pamoja na safari za viongozi wa nchi na watu mbalimbali walio katika nafasi za utawala.
Ni muhimu ukafahamu kuwa kuna safari za viongozi wa nchi ambazo huwa zina ratibiwa na shetani ili kuliharibu taifa na njia hii shetani anaitumia sana, kuratibu safari mbalimbali na ujio wa watu mbalimbali katika taiga kumbuka habari za Yusufu kukimbilia Misri akiwa na Mariamu mkewe pamoja na Yesu ilikuwa safari iliyoratibiwa na Mungu mwenyewe ili kumnusuru Yesu asiangamizwe na Herode,kama Mungu kuna safari anaziratibu nimuhimu uelewe kuwa hata shetani naye huwa anaratibu safari mbalimbali.

Kila safari huwa ina mambo mawili;sababu ya kusafiri na matokeo ya safari kwa hiyo shetani anaporatibu safari anakuwa na makusudi au sababu na pia anakuwa ameshapiga mahesabu juu ya matokeo ya safari hiyo katika taifa.
(2 MAMBO YA NYAKATI 18:1-34)
Tunaona Mfalme Yehoshafati aliondoka au alisafiri kwenda kumtembelea Mfalme Ahabu hiyo ilikuwa ni safari ambayo iliratibiwa na shetani kabisa na utaona alipofika kwa Ahabu ghafla Mfalme Ahabu anamshawishi Mfalme Yehoshafati ili amsaidie ili waende kupigana na maadui wa Mfalme Ahabu.
Baada ya Mfalme Yehoshafati kukubali kumsaidia Mfalme Ahabu kwenye vita yake jambo hilo halikumfurahisha Bwana ghafla Mfalme Yehoshafati anapata msukumo wa kutafuta nabii ili wamuulize Bwana kama waende vitani au wasiende.

MATOKEO YA SAFARI YA MFALME YEHOSHAFATI KWA TAIFA LAKE
1.Wanajeshi walikufa(2 mambo ya nyakati 18:3) Mfalme Yehshafati alipokubali kuwa atakwenda vitani kumsaidia Mfalme Ahabu tunaona Ahabu anakwenda na jeshi lake na wanajeshi walikufa vitani na hata yeye mwenyewe alinusurika kufa Bwana akamuokoa (2 mambo ya nyakati 18:31) chanzo cha hayo yote ni safari, ni muhimu sana kwa maaskari kuwa waombaji kwa sababu wao wanaishi kwa amri tu kwa hiyo lolote watakaloagizwa kufanya haijalishi ni jema au baya lazima walifanye tu na hata unapoangalia maaskari wengi wa nchi mbalimbali wanakufa Vitani kwa sababu ya mikataba iliyofanywa na viongozi wa nchi juu ya masuala ya ulinzi na usalama na ukiangalia mikataba mingi kama si yote chanzo chake ni safari.
2.Kuna familia katika taifa la Yuda lililokuwa likiongozwa na Yeshoshafati zilibaki na mzazi mmoja yaani mama tu(single parent family) hususani familia ambazo akina baba walikuwa wanajeshi(2 mambo ya nyakati 18:3,28) Mfalme Yehoshafati alipeleka wanajeshi vitani na wengine walikufa na hatimaye kwenye taifa zikabaki familia ambazo hazina baba bali ni mama ameachwa kuongoza familia kwa hiyo safari ya Mfalme Yehoshafati ilisababisha idadi ya wajane ikaongezeka katika taifa.
3.Baadhi ya familia zilijikuta kwenye hali ngumu za kiuchumi hususani familia za wanajeshi waliouawa vitani,yote hayo yalisababishwa na safari ya Mfalme Ahabu.
MATOKEO YA VITA KWA TAIFA LA SAMARIA
1.Taifa la Samaria lilipoteza Mfalme kwa sababu Ahabu alikufa vitani(2 mambo ya nyakati 18:15,34)

2.Kuna familia katika taifa la Samaria zilibaki na mzazi mmoja tu hususani familia za wanajeshi ambazo akina baba walikufa vitani maana yake ni kwamba idadi ya wajane iliongezeka Samaria.
3.Wanajeshi wengi walikufa na uchumi uliyumba si kwa familia tu ambazo zilipoteza wapendwa wao bali hata kwa taifa kwa sababu vita inatafuna hata uchumi wa taifa.

(1 WAFALME 16:29-33)
Mfalme Ahabu alioa mwanamke ambaye alitoka nje ya nchi na hii ilikuwa hatari kwa taifa la Israeli kwa sababu huyo mama ndiye alikuwa mke wa Mfalme na wakati huohuo ni muabudu miungu na ndio maana ni muhimu sana kumwombea mke au wake wa viongozi wa nchi kwa sababu ukiangalia kuna mambo mengine yalifanywa na yezebeli na kwa hali ya kawaida ungeweza kusema aliyefanya ni Mfalme kumbe si Mfalme bali ni mkewe.

MATOKEO YA SAFARI YA YEZEBELI KATIKA TAIFA LA ISRAELI
1.Yezebeli mke wa Ahabu alimfanya Ahabu ajenge madhabahu za miungu ya Baali katika taifa alilokuwa akiliongoza hivyo basi Mfalme Ahabu akawa muabudu miungu(1 Wafalme 16:29-33)

2.Maisha yakaanza kuwa magumu kwa watumishi wa Bwana, watumishi wa Bwana wakaanza kuuawa(1 Wafalme 17:13,19:2-10)

3.Taifa la Samaria likawa na wimbi kubwa la manabii wa uongo(1 Wafalme 18:21-22) kumbuka manabii wa uongo wakiongezeka katika taifa mafundisho ya uongo yanaongezeka na mafundisho ya uongo yakiongezeka ghafla na imani za watu zinageuka kuelekea kwa miungu iliyotoa mafundisho hayo kwa kuwa imani chanzo chake ni kusikia na imani za watu zikielekea miungu,miungu ndio itaabudiwa katika taifa.

4.Yezebeli aliingia katika taifa la Samaria na Miungu yake na ghafla hali ya mashaka ikatengenezwa ndani ya mioyo ya watu na hivyo basi watu wakaanza kuishi kwa mashaka juu ya Mungu wa Israeli(1 Wafalme 18:21).

5.Yezebeli alipoingia Samaria ghafla mbinu mpya za mauaji zikachukua nafasi katika taifa na wenye haki wakaanza kuuawa kwa ajili ya haki zao na ukiangalia muhuri uliotumika kuua wenye haki ni muhuri wa Mfalme lakini hakuweka mhuri Mfalme Bali aliyeweka muhuri ni mkewe na ndio maana nikakwambia kuwa ni muhimu kuwaombea wake za viongozi (1 Wafalme 21:1-13).


MATOKEO YA SAFARI ZA WANAWAKE AMBAO WALIINGIA KATIKA TAIFA LA ISRAELI
1.Wanawake walioingia kwenye taifa la Israeli,wanawake aliowependa Mfalme Sulemani walimgeuza moyo alipokuwa mzee na hakumfuata Bwana Bali miungu.
(1 Wafalme 11:4)
Jambo la kujifunza:Wanawake wale walimgeuza moyo alipokuwa mzee,maana yake ni kwamba shetani aliwategesha pale kwenye taifa kwa muda na baadae wakawa mtego kwa Mfalme, ni muhimu ukafahamu kuwa ni muhimu sana kuiombea idara ya uhamiaji hususani katika suala la utoaji vibali vya kuishi nchini ili Mungu awawezeshe katika masuala ya utoaji wa vibali ili wasije wakampa kibali mtu ambaye ameletwa na shetani katika taifa ili awe mtego kwa taifa.

2.Wanawake wageni walimfanya Sulemani akajenga madhabahu za miungu katika taifa jambo ambalo ni machukizo kwa Bwana.
(1 Wafalme 11:7)
Kumbuka Mfalme anapojenga madhabahu za miungu hajengi kwa pesa same za mfukoni Bali anatumia rasilimali za taifa kwa hiyo kwa kufanya hivyo anaukabidhi uchumi wa taifa kwa miungu na si ajabu kukuta bajeti kubwa inaelekezwa kwenye ujenzi wa viwanda vya pombe,sigara,upanuzi wa magereza n.k na taifa zima linaingia kwenye hatia ya kuabudu miungu.

3.Ufalme wa Sulemani,Mungu aliugawanya lakini ni katika siku za mwanae(1 Wafalme 11:11-12)maana yake ni kwamba taifa liligawanyika lakini kosa lilifanywa na Mfalme Sulemani.
(1 Wafalme 11:9-11)
Jambo la kufahamu jaribu kuchunguza mataifa mbalimbali yaliyogawanyika;Sudani,Korea n.k ni rahisi sana kukuta chanzo cha mgawanyiko ilikuwa ni safari mbalimbali kwa mfano unaweza kukuta kiongozi alisafiri na katika ziara yake akanyweshwa maneno na aliporudi akaongoza mapambano ya kupindua serikali,fuatila kuhusu mataifa mbalimbali kwa mfano Uganda utaona Raisi Milton Obote aliwahi kuishi hapa Tanzania na akatengenezwa na aliporudi Uganda akachukua nchi kijeshi. 

4.Mfalme Sulemani akataka kumuua Yeroboamu mtu ambaye Bwana alimuandaa kuwa Mfalme,maana yake ni kwamba baada ya Sulemani kugeuzwa moyo wake ghafla akawa na uchu wa madaraka hivyo basi hakuwa tayari kuona mtu baki akiwa Mfalme ingekuwa kwa nyakati za sasa tungeweza kusema kuwa Raisi hayuko tayari kuachia madaraka kwa mtu asiye wa chama chake anachohitaji ni kwamba hata akitoka madarakani atawale mtu wa kutoka kwenye chama chake.
Ni muhimu sana kuombea safari za watu mbalimbali iwe viongozi au wasio viongozi kumbuka yote hayo uliyoyasoma yalitokana na safari za viongozi na wasio viongozi.

MAMBO KADHAA YA KUOMBEA JUU YA SAFARI ZA VIONGOZI NA WASIO VIONGOZI MAADAMU WANAINGIA NA KUTOKA KATIKA NCHI HUSIKA
1.Ombea mipaka isipitishe kitu chochote kisicho cha mapenzi ya Mungu
(Mathayo 16:19)

2.Kwa njia ya MAOMBI,funga safari zote za ndani na nje ambazo zimeratibiwa na shetani (Mathayo 16:19)

3.Ikiwa shetani kuna watu amewategesha nchini kwako kwa makusudi fulani,omba Mungu awarudishe walikotoka(1 Wafalme 11:1-4) umeshawahi kufikiri juu ya wapelelezi ambao Musa aliambiwa na Mungu waende waipeleleze nchi ya Kanaani(Hesabu 13) ni Mungu aliwatuma kupitia MUSA basi ni vema uelewe kama Mungu alimwagiza Musa kuwatuma watu kupeleleza, ni ujue na shetani naye huwa anachomeka watu katika taifa wanaingia kama wageni na sio kwamba ni wageni kweli Bali wanaingia kutekeleza kusudi la shetani, jaribu kuwauliza waKenya juu ya shambulio la soko la kimataifa la West gate Mall,ukifuatilia tukio hilo utaona magaidi waliingia wakitokea Somalia na wakafanya uharibifu mkubwa sana.

4.Omba Mungu avunje umoja uliotengenezwa na shetani, kumbuka shetani alimuunganisha Mfalme Yehoshafati na wakaunganisha nguvu za kijeshi ili waende vitani(1 Mambo ya nyakati 18:1-34) matokeo yake kuna madhara makubwa yalitokea, umewahi kujiuliza juu ya miunganiko mbalimbali kama SADC,COMESA,UN,EAC(japo miunganiko ya namna hii haiwezi kuvunjika kwa kuwa inatokea kwa kuwa tunaelekea mwisho wa dunia) umeshawahi kujiuliza ni nani muhasisi wake? Unayajua malengo yake? Umeshawahi kujiuliza faida na hasara zake? Umeshawahi kutathmini matokeo ya miunganiko hiyo kwa ngazi ya taifa na maisha ya mtu mmojammoja kiroho na kimwili?

Chapisha Maoni

0 Maoni