MKOLONI NDANI YA TAIFA HURU





Na Faraja Gasto
0767955334

 Lengo la sura: ni kukuonyesha madhara ya mifumo ya kikoloni kwenye taifa huru.
Wote tunafahamu kuwa kama mkubwa yupo basi na mdogo yupo kwa kuwa hakuna mkubwa asiye na mdogo, wakoloni walikuwa kama wakubwa nasi tukawa kama wadogo pindi walipotuweka katika mikono yao, walituwekea taratibu za kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuvaa, kuoa, kujifunza n.k na kwa kuwa tulilainishwa kwa maneno matamu na ulaghai wa kutumia vioo vya kujitazama nyuso zetu, vikoi na vitu vingine tukaamua kuwa bendera zilizofuata upepo kwa kufanya kile ambacho tuliongozwa kufanya, oooooooh “tukawa watumwa kwenye nchi zetu wenyewe”.
Kadri siku zilivyozidi kwenda ndipo tukaanza kujitambua lakini tulikuwa tumechelewa, kwani wakati tulipojitambua tulikuwa tumeshanyonywa vya kutosha na hapa ndipo likaanza fukuto la kutaka uhuru, wakati huo ndipo wakaanza kuinuka wapigania uhuru ambao walibahatika kupata elimu na macho yao ndipo yakaanza kuona kuwa tunanyonywa, wakaanza kuudai uhuru ambao waliukopesha kwa wakoloni kutokana na ukosefu wao wa elimu na kupenda kufanyiwa kila kitu badala ya kuthubutu kufanya na mwisho wa siku tunajiuliza “kwani wao waweze wana nini hata sisi tushindwe tuna nini?”.
Tulipopewa vioo tukatazama nyuso zetu tukaamua kuhonga vito vya thamani ambavyo vilitumiwa na waliojua kuvitumia kustawisha na kuendeleza nchi zao na huku nchi zetu zikiwa katika hali ya umaskini uliokithiri ilihali tulikuwa na viondoa umaskini.
“enyi waafrika ni nani aliyewaroga?”
Hata baada ya kuupata uhuru tulioukopesha kwa wakoloni tukajikuta tumeshindwa kuutumia uhuru tulionao kama ilivyotupasa kuutumia na hapo ndipo ukawa mwanzo wa ukoloni mamboleo, japo tukautangazia umma kuwa tuko huru lakini tukawa huru midomoni lakini tukabaki kuwa watumwa nafsini tulirithi mifumo ya wakoloni bila kuihariri. Mifumo tuliyoachiwa ilikuwa imetengenezwa ili kutufanya tuendelee kuwa watumwa wa wakoloni na kama mifumo hiyo ilitengenezwa ili kutunyonya na walioitengeneza wakatuachia je! sio mwanzo wa kunyonyana sisi kwa sisi?
Nakumbuka waliotangulia kuliona jua kabla ya wanaoliona jua walisema “ukipewa akili za mwenzako changanya na za kwako”. Kitu tulichokosa kwa muda mrefu ni kuchanganya akili zetu za zile tulizoachiwa ili tuweze kupata mifumo ambayo inatufaa kwa wakati wetu na kwa mazingira yetu ya hapa Afrika. Kutokana na kutokuihariri mifumo tuliyoachiwa na wakoloni ndio maana leo hii nchi za Afrika zimekuwa zikiombaomba misaada kutoka kwa wakoloni, ni jambo la kushangaza kuomba mali yako kwa kuwa walituchukulia rasilimali zetu na mwishowe tunapozihitaji inatubidi tukunje goti tuwaombe na kabla hawajatupatia wanatupa masharti yanayokinzana na maadili yetu kwa mfano tukubali wanawake waoane wao kwa wao, wanaume waoane wao kwa wao, kutoa mimba iwe ruksa, mume ambaye ni kichwa cha mke awe kama mwanamke ndani ya nyumba n.k na kwa kuwa hatuna namna ya kufanya tumejikuta tunakubaliana na hayo wanayotaka na hapo ndipo mkono wa mkoloni ulipofanikiwa kurudi tena katika bara letu la Afrika.
Mifumo ya kikoloni imekuwa dhahiri kwenye nchi zetu za Afrika na inatutesa sana japo si kila mfumo ni mbaya ila mifumo iliyo mingi haitufai kwa nchi zetu za Afrika na kwa kuwa ndivyo tulivyochagua kuwa huru midomoni na huku tukiwa watumwa nafsini mwetu basi ndio maana tuko hivi tulivyo leo, hakuna utumwa mbaya kama utumwa wa nafsi, utumwa wa nafsi unamfanya mtu awaze kusaidiwa kila anapohitaji kufanya jambo Fulani haijalishi ni dogo au kubwa, utumwa na nafsi unamfanya mtu asiwe na muda wa kukaa chini na kufikiri vya kutosha juu ya mambo mbalimbali hali kadhalika utumwa wa nafsi unamfanya mtu aamini kila neno bila kulichunguza na haya ndiyo tunayoyashuhudia kwenye nchi zetu za Afrika, imefikia hatua fikra za waliotutawala zinaaminika sana na zinatumiwa sana kushughulikia mambo ya nchi zetu, japokuwa sipingi kila kitu kinachotoka kwenye mataifa ya wenzetu weupe lakini natafakari jambo hili ukienda kwenye vyuo vyetu utakuta vitabu vingi vimejaa vya waandishi wa kutoka Asia, Ulaya na bara la Amerika ya kusini na kaskazini, swali tunajiuliza je! hakuna wasomi wa kiafrika wanaoweza kuandika vitabu vitakavyowasaidia watoto na vijana wetu kuongeza maarifa kulingana na tafiti zao, uvumbuzi wao na kulingana na mazingira yetu ya hapa Afrika?. Mkoloni amerudi Afrika kimyakimya japo waafrika hawataki kuukubali ukweli huu lakini huwezi ukaupinga ukweli kwa mtazamo au hisia kwa kuwa “mwenye macho haambiwi tazama”.
Tufanye nini?
1.Tuihariri mifumo tuliyoachiwa na wakoloni.
Ninaposema kuihariri mifumo namaanisha tuna wajibu wa kuangalia nini walichotuachia wakoloni kinachotufaa na ambacho hakitufai kulingana na maadili yetu na mazingira yetu.
2.Tujikubali kuwa tunaweza.
Njia mojawapo ya kuushinda utumwa wa nafsi ni kujikubali kuwa hata wewe unaweza kufanya yanayofanywa na waliotangulia kufanya, ni muhimu tuwakubali wataalamu wetu wa ndani kwani wakipewa nafasi ya kutumia uwezo, ujuzi na maarifa waliyonayo lazima tutaona mabadiliko makubwa kwenye nchi zetu za Afrika.
3.Tufikiri vya kutosha.
“Ulivyonavyo vinatosha ikiwa utafikiri vya kutosha” ni sentensi iliyowahi kusemwa na Askofu David Oyedepo. Kinachotuponza katika nchi zetu za Afrika ni kutokaa na kufikiri vya kutosha, jaribu kuangalia rasilimali tulizonazo na maisha tunayoishi ni vitu viwili tofauti, kabla ya kuamua kuomba msaada nje lazima tukae chini kwanza tufikiri vya kutosha huku tukikumbuka “akopaye ni mtumwa wa akopeshaye”.
4.Tukubali ukweli.
Kipimo kimojawapo cha ukomavu wa kifikra ni kuubali ukweli, ukweli ndio unaomfanya mtu kuwa huru kwelikweli lakini pale inapofikia hatua tuukakataa ukweli basi tutarajie kuwa watumwa siku zote, na ni muhimu tukumbuke kuwa ukweli hauna dini, kabila, chama n.k kwa kuwa kila mwanadamu anaweza akasema ukweli lakini katika nchi zetu za Afrika mtu akionekana yuko kwenye chama pinzani basi kinakuwa kigezo tosha kuwa hawezi kusema ukweli jambo ambalo sio sahihi.
5.Tuaminiane.
Kutoaminiana ni jambo ambalo linaharibu mambo mengi katika nchi za Afrika, imekuwa si ajabu kuona watu walio kwenye vyama tawala hawana imani na walio kwenye vyama pinzani na walio kwenye vyama pinzani hawana imani na walio kwenye vyama tawala, tukifikia hatua ya kuaminiana tutarajie kuona mbadiliko makubwa sana kwenye nchi zetu za Afrika.

Chapisha Maoni

0 Maoni