MAOMBI KWA AJILI YA HALI ZA KIROHO ZA MAENEO



Kuombea maeneo si jambo ambalo linakumbukwa na watu wengi na matokeo yake maeneo yamekuwa na hali mbaya sana za kiroho, unaposoma Biblia utaona Mungu aliwaambia wana wa Israeli “wautakie AMANI MJI waliotoka” yaani wauombee amani mji wao maana mji unapokuwa na amani ndipo na wao watapata amani kutokana na amani ya mji (Yeremia 29:7).
Mara nyingi tumekuwa tukisikia kuhusu “utabiri wa HALI ya hewa” na katika utabiri wa hali ya hewa ndipo wataalamu huwa wanatuambia kuwa eneo Fulani kutakuwa na hali Fulani kwa mfano joto kiasi, mvua kiasi, mvua zinazoweza kuleta madhara n.k na wakati mwingine wataalamu hutoa maelekezo juu ya namna ya kujikinga na hali ambayo inaweza kutokea kutokana na hali iliyotabiriwa.

Ndivyo ilivyo hata katika masuala ya kiroho, roho Fulani inapokaa juu ya eneo ghafla hali ya hali ya eneo inabadilika kabisa itategemeana na roho iliyokaa juu ya eneo ni roho ya aina gani, na kama roho hiyo haitokani na Mungu basi lazima hali itakayokuwepo juu ya eneo itakuwa hali yenye madhara makubwa juu ya eneo na juu ya maisha ya watu endapo haitashughulikiwa kwa njia ya maombi.
Ninaposema kuombea hali za kiroho za maeneo ninalenga kushughulikia roho zinazopata nafasi ya kukaa juu ya eneo Fulani na zinasababisha madhara katika mazingira na maisha ya watu kwa ujumla, tumekuwa tukishuhudia mitaa, vijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa au taifa likiwa na sifa Fulani kwa mfano unaweza ukasikia mtaa au kijiji Fulani kuna wachawi wengi au kuna makahaba wengi au mabinti wengi huwa hawamalizi masomo au kuna wavuta bangi wengi n.k chanzo kimojawapo cha matukio hayo ni hali za kiroho za maeneo husika.

(Mwanza 1:1-2)
Ukisoma andiko hilo utakutana na sentensi hii “Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji            Biblia inasema Giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji maana yake ni kwamba ili giza liondoke juu ya uso wa vilindi vya maji ilitakiwa kwanza Roho ya Mungu ije juu itulie juu ya uso wa maji na baada ya Roho ya Mungu kuja juu ya uso wa maji ndipo Mungu akasema “iwe nuru na nuru ikawa”. Ninachotaka uone hapo ni suala la Roho ya Mungu na mazingira, kwa hiyo ni vema ujue hata roho za kishetani zinaweza kukaa juu ya eneo na ghafla matokeo ya uwepo wa ile roho yataanza kutokea kwenye mazingira na maisha ya watu kwa ujumla kutokana na hali ya kiroho itakayotengenezwa na ile roho.
Badhi ya mambo yanayotokea pale roho Fulani inapokaa juu ya eneo
àHali ya kiroho ya eneo huwa inatengeneza AINA FULANI YA WATU
Kwa mfano watu wachoyo, wasio wakarimu, wafiraji, makahaba, wapenda rushwa n.k. Ukiona mtu anaitwa MASKINI ni vema ujue kinachofanya aitwe hivyo ni HALI aliyonayo yaani UMASKINI ndio unatengeneza watu MASKINI, kumbuka UMASKINI ni roho inayotokana na shetani, kwa hiyo kama roho ya umaskini itakaa juu ya eneo tarajia kuona eneo hilo likikaliwa na watu maskini.

(Matendo ya mitume 21:39)
Mtume Paulo anasema alitoka katika “MJI USIOKUWA MNYONGE” unaweza ukajiuliza Paulo alikuwa anamaanisha nini kusema kauli hiyo, ukisoma hilo andiko kwa haraka unaweza usione maana ya hiyo sentensi lakini Mtume Paulo alikuwa anazungumzia hali ya kiroho ya MJI aliotoka.
Kwa hiyo Paulo anataka wau wajue kuwa hali ya kiroho ya eneo inatengeneza na aina Fulani ya watu na ndio maana Mtume Paulo alikuwa mtu jasiri hakuwa mtu goi goi na ndio maana hata alipokuwa muuaji alifanya kazi yake kwa uhodari mkubwa na hata alipokuwa mtumishi wa Mungu alikuwa mtumishi mwenye uhodari na hata kuna mahali aliwaandikia watu “hatimaye MZIDI KWA HODARI katika Bwana”. Kilichomtengeneza Paulo kuwa mtu jasiri ni hali ya kiroho ya mji aliotoka.

Hali ya kiroho ya eneo huwa inatengeneza AINA FULANI YA MATUKIO katika eneo husika.
Kwa mfano kuna maeneo mengine si ajabu kuona ajali zikitokea mara kwa mara, wizi wa mara kwa mara, watoto kutupwa majalalani n.k hayo yote yanasababishwa na hali ya kiroho ya eneo husika.
(Isaya 1:21-27)
Tunaona katika andiko hilo Mungu anasema kuwa “MJI HUO ULIKUWA MWAMINIFU” lakini ghafla “MJI UMEKUWA KAHABA” ukisoma andiko hilo kwa haraka unaweza usione maana ya andiko hilo lakini unaposoma andiko hilo kwa msaada wa Roho Mtakatifu utagundua kuwa hapo awali uaminifu ulitawala katika mji na kutokana na uaminifu wa mji ukapelekea na watu waliokuwa wanaishi katika mji wakawa waaminifu, lakini baada ya muda “roho ya ukahaba” ikapata nafasi juu ya mji, sasa angalia matukio yaliyoanza kutokea baada ya hali ya kiroho kubadilika, nataka nikuonyeshe matukio machache;
(a)Fedha yao haikuwa na thamani(thamani ya fedha ilishuka) hali ya kiroho ya mji ilipobadilika ghafla na thamani ya fedha ikashuka, hili suala la thamani ya fedha kushuka si suala geni kwa kuwa linaonekana hata leo unakuta sehemu nyingine mtu anakwenda na hela nyingi sokoni lakini anarudi amenunua vitu vichache kwa kuwa thamani ya fedha imeshuka na hicho ndicho kilichotokea hali ya kiroho ilipobadilika katika eneo lile (Isaya 1:22)
(b)Suala la kutenda haki likatoweka katika mji, maana yake ni kwamba dhuluma ikatawala katika mji (Isaya 1:21)
(c)Viongozi wakaanza kuwa waasi na marafiki wa wezi, viongozi wakaanza kuwa na marafiki mafisadi (Isaya 1:23)
(d)Rushwa ikaanza kutawala (Isaya 1:23)
Hayo yalikuwa baadhi ya matukio yaliyotokea baada ya hali ya kiroho ya mji kuwa imebadilika.

Hali ya kiroho ya eneo inaweza kuwafanya watu waliopo kwenye eneo hilo wakawa wanaota aina Fulani ya ndoto kulingana na roho iliyokaa kwenye eneo
(Mwanzo 28:10-17)
Tunaona katika andiko hilo Yakobo alifika mahali Fulani akalala na baada ya kulala akaota ndoto ambayo ilidhihirisha kuwa Mungu yuko mahali pale, na baada ya ndoto hiyo Yakobo anasema hakujua kuwa Mungu yuko mahali pale na Yakobo akahisi kwamba lile eneo ni LANGO LA MBINGUNI kwa kuwa Mungu alijifunua kwake kwa njia ya ndoto.
Ninachotaka uone hapo ni kwamba roho Fulani ikikaa juu ya eneo ghafla watu wa eneo husika wanaweza kujikuta wakiota ndoto zinazofanana.

Hali ya kiroho ya eneo huwa inatengeneza AINA FULANI YA TABIA
(Danieli 3:1-7)
Tunanona katika wilaya ya Babeli kuabudu miungu ilikuwa ni jambo la kawaida kwa kuwa ilifikia hatua kuabudu miungu ikawa tabia yao, hiyo yote ilitokana na hali ya kiroho ya eneo husika, tunaona akina Shadraka na wenzake walipokuja kuonyesha tabia tofauti na tabia ya eneo husika ghafla wakatangaziwa kuuawa.
(Mwanzo 20:1-3)
Tunaona watu wa lile eneo walikuwa na tabia ya kuchukua wake za watu kwa nguvu na kulala ndio maana Ibrahimu akaona aseme kuwa Sara ni dada yake na si mke wake kwa kuwa Ibrahimu aliogopa kuuawa kwa kuwa watu wa lile eneo walikuwa na tabia ya kuua kila mwanamume mwenye mke mzuri.
Kwa hiyo ni vema kila mwana wa ufalme ajue anao wajibu wa kuomba kwa ajili ya mambo mbalimbali katika nchi na taifa kwa ujumla.

Chapisha Maoni

0 Maoni