FARAJA GASTO
Utangulizi
“Huwezi kuwa msaada kwa
watu kama haujawa msaada kwako wewe mwenyewe”
Watu wengi wanapenda
sana kuwa msaada kwa watu lakini wanashindwa kwa kuwa hawajawa msaada kwao
wenyewe, labda unaweza kujiuliza namaanisha nini. Nataka nikupe mifano kadhaa
ili uweze kunielewa, kwa mfano kama wewe huna pesa huwezi kumpa mtu mwingine
pesa, kama wewe huamini kama Yesu anaweza huwezi kuwa na ujasiri kumwambia mtu
mwingine kuwa Yesu anaweza, kama wewe haujui umuhimu wa elimu huwezi ukamwambia
mtu mwingine umuhimu wa elimu.
Kwa hiyo lazima ufahamu
vizuri misingi ya kuwa msaada kwa wengine kwa mujibu wa Biblia.
Msingi
wa kwanza
Anza
kujitengenezea mazingira wewe mwenyewe(wewe kwanza)
(Luka
22:31-33)
Yesu alimwambia Petro
“utakapoongoka waimarishe wengine” maana yake ni kwamba Petro alitakiwa kuwa
imara yeye kwanza ili aweze kuwaimarisha wengine, kwa hiyo ili uwe msaada kwa
watu lazima wewe mwenyewe uanze kujitengenezea mazingira wewe kwanza.
Kumbuka huwezi kuwaza
kwa ajili ya wengine kama wewe mwenyewe haujawa vizuri katika eneo Fulani,
maana yake ni kwamba huwezi kutoa kitu ambacho hauna. Huwezi kuwabadilisha
wengine kama wewe haujabadilika ndio maana Mtume Paulo alimwandikia Timotheo
kuwa aanze yeye kuwa kielelezo kwa usemi, mwenendo, upendo, imani na usafi,
maana yake ni kwamba kama yeye hajawa kielelezo basi hata anaowaongoza hawawezi
kuwa na mwenendo mzuri.
Msingi
wa pili
Unataka
uwe msaada kwa watu gani(wengine)
(Luka
19:10)
Hili lazima ujiulize,
unataka kuwa msaada kwa watu wa aina gani, unapojiuliza hilo swali utagundua
kuwa kila watu wana aina Fulani ya uhitaji. Kumbuka Yesu alikuja kutafuta na
kuokoa kile kilichopota, kwa hiyo waliopotea hao ndio Yesu aliwalenga.
Msingi
wa tatu
Yajue
mahitaji ya watu unaotaka kuwa msaada kwao
(Yohana
1:17)
Yesu alipokuja na
ajenda ya kuwatafuta wale wote waliopotea alijua nini ambacho wanakihitaji ndio
maana Biblia inasema alikuja na “Neema na Kweli” kwa hiyo unapohitaji kuwa
msaada kwa wengine lazima ujue wanahitaji nini.
Msingi
wa nne
Je!
unacho wanachokihitaji watu unaotaka kuwa msaada kwao? Na kama hauna una nini?
(Matendo
ya mitume 3:1-8)
Siku moja wakati nikiwa
natoka darasani nilikutana na dada mmoja amebeba mtoto wake mgongoni na Yule
dada alikuja karibu yangu na kuniambia nimsaidie kiasi fulani cha fedha kwa
kuwa mtoto wake alikuwa anaumwa lakini kwa wakati huo sikuwa na pesa ikabidi
yule dada aondoke, ukatokea wakati fulani nikawa nazungumza na mtumishi wa
Mungu Fulani juu ya hilo suala na aliniambia kitu ambacho bado nakikumbuka, Yule
mtumishi aliniambia “kama haukuwa na pesa ilikuwaje ukashindwa kuweka mikono
juu ya Yule mtoto na kumuombea” aliponiambia hilo suala lilinipa kufikiri
kidogo. Ninachotaka nikuambie ni kwamba kama unahitaji kuwa msaada kwa wengine
lazima utafute na upate kile ambacho wanakihitaji hao watu na kama hauna
wanachohitaji lazima uwe na kitu cha ziada.
Kiwete aliyekuwa kwenye
mlango wa hekalu alikuwa akitaka kupewa fedha lakini Mtume Petro akamwambia
kuwa “sina fedha wala dhahabu” lakini japokuwa Petro hakuwa na fedha wala
dhahabu alikuwa na kitu cha ziada ambacho kingemfaa zaidi ya fedha, Mtume Petro
alikuwa na jina la Yesu na alipolitaja jina la Yesu lilileta matokeo makubwa
zaidi ya fedha.
N.B kuna wakati unaweza
ukawa hauna fedha lakini ukawa na kitu cha ziada zaidi ya fedha kwa mfano
mawazo n.k
Msingi
wa tano
Uwe
tayari kuchukua maamuzi magumu
(Wafilipi
2:4-7)
Biblia inasema
tuyaangalie mambo ya wengine, jaribu kufikiri una shilingi mia tano na kuna mtu
amekujia ana shida na shilingi mia tano na ukimtazama unamuonea huruma kabisa
lakini moyoni unabaki unawaza kuhusu wewe mwenyewe pesa uliyonayo ndio hiyohiyo
na laiti kama ungekuwa na uhakika wa kupata nyingine basi ungeweza kumpa,
lakini sasa na wewe una hiyohiyo na hauna uhakika wa kupata nyingine. Kwa
mazingira ya namna hiyo ndipo suala la maamuzi magumu linapokuja, Biblia
inasema Yesu alikuwa tayari kuchukua maamuzi magumu ya kuacha enzi na utukufu
aliokuwa nao na akaja kuishi kama mtu wa kawaida ili awe msaada kwa wengine.
Kuna wakati Mungu huwa
anataka kitu cha pekee yaani kitu ulichonacho na hauna uhakika wa kupata
kingine, kumbuka hata Mungu kuna wakati huwa anachukua maamuzi magumu na ndio
maana Biblia inasema alipoupenda ulimwengu alimtoa”mwanawe pekee” ili kila
amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele(Yohana 3:16) kwa hiyo suala la
maamuzi magumu haliepukiki maadamu unaishi. Ukisoma habari za Ibrahimu
utagundua kuna wakati Mungu alimjaribu Ibrahimu kwa kumtaka amtoe mwanawe wa
pekee (Isaka) ulikuwa ni wakati mgumu sana kwa Ibrahimu lakini Ibrahimu
alichukua maamuzi magumu na akawa tayari kumchinja Isaka lakini Mungu alipoona
hilo jambo alimzuia Ibrahimu.
Unapohitaji kuwa msaada
kwa wengine lazima uwe tayari kufanya maamuzi magumu kwa kutoa ulivyonavyo ili
wengine wapate faida.
Msingi
wa sita
Lazima
uwaze faida ya wengine kabla ya faida yako
(Wafilipi
2:6-11)
Unapohitaji kuwa msaada
kwa wengine utajikuta vipaumbele vyako vimebadilika, badala ya kuwaza faida
yako kwanza utatakiwa kuwaza faida yaw engine kwanza, yaani unafika mahali unasema
kama utapata faida sawa kama hautapata faida sawa. Lakini ni vema ujue huwezi
ukawa msaada kwa wengine halafu Mungu akakuacha jinsi ulivyo lazima Mungu
atafanya kitu kwa ajili yako.
Yesu alipofanyika
ukombozi kwa ulimwengu, Mungu alimkirimia jina lile lipitalo majina yote na ili
kwa jina la Yesu kila goti lipigwe la vitu vya mbinguni na vya dunia na vya
chini ya nchi.
Msingi
wa saba
Usiwe
msaada ili upate sifa na utukufu bali sifa na utukufu muachie Mungu pekee
(Mathayo
6:1)
Ikiwa utahitaji kuwa msaada
kwa wengine ili upate sifa na utukufu utakuwa unakosea sana, unapohitaji kuwa
msaada kwa wengine lazima nia yako iwe kama nia ya Yesu Kristo(Wafilipi 2:5)
yaani unafanya kwa ajili ya utukufu wa Mungu, Yesu alipokuja duniani kwa ajili
ya ukombozi hakujua kuwa baada ya kazi aliyotakiwa kuifanya alikuwa ameandaliwa
jina lipitalo majina yote, lakini alikuja kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wa
Mungu lakini baada ya kazi alipata zawadi ambayo nadhani hata yeye alishangaa,
na ndhani hata malaika waliitamani sana zawadi aliyopata Yesu Kristo, alipewa
heshima ya ajabu lakini alifanya kazi huku akiwa na nia ya kumletea Mungu Baba
utukufu ndio maana maandiko yanatuambia na sisi tuwe na nia hiyohiyo ambayo
ilikuwemo ndani ya Kristo Yesu.
Mungu akubariki kwa
kuwa umeelewa.
Ni mimi nduguyo
FARAJA GASTO
0767955334
0 Maoni