FANYA MAMBO KWA BIDII




“Bidii na umasikini ni sawa na paka na panya”
Bishop Augustine Mpemba

SWALI: Je! umemuona mtu mwenye bidii(juhudi) katika kazi zake?
Mtumishi wa Mungu huyo aliyesema kauli hiyo hapo juu anataka ujue kuwa bidii na umaskini havikai nyumba moja kama jinsi ambavyo paka na panya hawawezi kukaa pamoja kwa hiyo kama mtu hana bidii katika mambo yake basi umaskini utakuwa fungu lake au umaskini utakuwa rafiki yake.
Hapo juu nimeanza kwa kukuuliza swali na hilo ni swali ambalo limo ndani ya biblia katika kitabu cha (Mithali 22:29)
Biblia inataka ujue kuwa mtu yeyote mwenye bidii(bidii) hawezi akawa maskini hata kama mtu huyo ni mpagani maadamu ameweka bidii(juhudi)  katika mambo yake lazima atafanikiwa tu kwa kuwa bidii(juhudi) ni rafiki wa mafanikio.
Ukisoma biblia utaona neno bidii limetajwa mara nyingi sana na biblia imeainisha maeneo ambayo mtu atatakiwa kuweka bidii(juhudi) katika kuyafanya.

1.      Kazi
(Mithali 22:29)
Watu wengi hawafanikiwi kwa kuwa ni wavivu wa kufanya kazi, wanapofanaya kazi hawafanyi kwa bidii, usipofanya kazi kwa bidii maana yake ni kwamba unafanya kazi kwa mkono mlegevu, ni vema ujue kati ya vitu ambavyo Mungu anavichukia ni ulegevu ndio maana maandiko yanasema “atendaye kazi kwa mkono mlegevu huwa maskikni” (Mithali 10:4) kwa hiyo kila mtu lazima afahamu kuwa umaskini si mpango wa Mungu ila ni maamuzi ya mtu yaani mtu ndiye anaweza akaamua awe maskini au awe tajiri na kitu kimojawapo kitakachokufanya uondokane na umaskini ni BIDII.
Watu wengi wamefukuzwa kazi kwa sababu ya kutokuwa na bidii, watu wengi wameshindwa kupandishwa vyeo kwa sababu ya kukosa bidii, ni vema ujue bidii yako ikionekana lazima utapata upendeleo kwa bosi wako, kama uko kwenye huduma bidii yako ikionekana lazima Mungu atakuinua, kwa hiyo unapofanya kazi zako lazima ufanye kwa BIDII.
Katika kipengele hiki kinachohusu kufanya kazi kwa bidii napenda kukihitimisha kwa kukukumbusha kitu ambacho amewahi kusema Raisi wa Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Kila mtu hupenda maendeleo lakini watu wengi hawajui mahitaji ya msingi yanayosababisha maendeleo, hitaji kubwa ni kufanya kazi kwa BIDII”
J.K Nyerere (1967), Uhuru na Ujamaa(uk, 244).

2.      Kusikia sauti ya Mungu na kutendea kazi maagizo yake
(Kumbukumbu la torati 28:1)
Mungu ameahidi kwa mtu yeyote ambaye ana bidii ya kuisikia sauti yake na kutendea kazi maagizo yake, Baraka zitakuwa zikimtafuta yeye yaani Baraka zitakuwa zikimkimbilia kwa kuwa Baraka zimeamriwa ziwajie watu wote wenye bidii ya kuisikia sauti ya Mungu na kutendea kazi maagizo ya Mungu.
Ni muhimu ujifunze neno la Mungu wewe binafsi na usisubiri kulisikia neno la Mungu kwenye mahubiri au semina kwa sababu kujifunza neno la Mungu ni njia mojawapo ya kusikia sauti ya Mungu na baada ya kujifunza neno la Mungu lazima ulitendee kazi hilo neno ulilojifunza. Neno la Mungu haliwasaidii watu wengi kwa kuwa wengi hawalitendei kazi neno, neno la Mungu litatenda kzai maishani mwako pale utakapoliingiza kwenye matendo na utakapoanza kulitendea kazi utashangaa nguvu iliyomo kwenye neo la Mungu. 

3.      Kuomba
(Yakobo 5:16-17)
Kuna watu wa aina mbili ambao wanapungua duniani (i) waaminifu (ii) waombaji. Watu wengi wamekuwa wavivu kwenye maombi na hili linadhihirika wazi makanisani, linapokuja suala la maombi utashangaa watu hawana hamu ya kuomba, maandiko yanasema kwamba Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi lakini kwa kuwa alikuwa na bidii(juhudi) ndio maana aliomba na matokeo yake mvua ikanyesha baada ya miaka mitatu.
Katika kuomba lazima uombe kwa bidii, bidii itakufanya usikate tamaa au usichoke mpaka uone kile ambacho umetamani kuona kinatokea, Eliya aliomba mara saba ndipo mvua ilitponyesha, bidii iliyowemo ndani yake ndio ilimfanaya asikate tamaa katika kuomba kwake, aliomba mara ya sita mvua haikunyesha ila alipoomba mara ya saba ndipo dalili ya mvua ikaonekana, kilichomfanya Eliya asikate tamaa ni BIDII.

Chapisha Maoni

2 Maoni