Ili ufanye tafakari zenye tija kuna mambo ya msingi unapaswa kuzingatia, mambo hayo ni nguzo au funguo muhimu za tafakari, nguzo mojawapo au funguo mojawapo ni kujiuliza maswali (kujiuliza wewe mwenyewe au kujiuliza nyie wenyewe).
Rejea mifano ifuatayo;
1. Mwana mpotevu (Luka 15:17)
Alijiuliza "ni watumishi wangapi wa baba yangu wanakula na kusaza na mimi hapa ninakufa kwa njaa"
Swali hilo lilimuingiza kwenye tafakari ambayo ilizaa maamuzi yaliyobadilisha maisha yake kabisa (Luka 15:20-23).
2. Wakoma wanne (2 Wafalme 7:3-8)
Hawa wakoma waliulizana "mbona tunakaa hapa tufe" swali hilo liliwaingiza kwenye tafakari iliyozaa maamuzi yaliyobadilisha maisha yao kabisa.
3. Wasafiri waliokuwa wanakwenda ninawi (Yona 1:7-15)
Hawa wasafiri walijikuta kwenye hali ngumu kutokana na bahari kuchafuka, walipofanya jitahada za kujiokoa na jitihada zikashindikana walitaka kujua chanzo cha tatizo hilo ni nini.
Swali lililowaingiza kwenye tafakari ni hili "mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani" swali hilo lilizaa tafakari iliyowapa mbinu za kumbaini mtu ambaye amesababisha bahari kuchafuka.
Mbinu yenyewe ilikuwa kupiga kura, kura yenyewe ilipigwa hivi.
Waliangalia ushiriki wa kila mtu kwenye harakati za kujiokoa, wakati wengine wanahangaika kujiokoa Yona alikuwa amelala, kwa hiyo Yona ndiye ambaye hakushiriki harakati za kujiokoa kura ikamwangukia Yona kwamba yeye anajua chanzo cha tatizo.
Walipomuhoji Yoha alikiri kuwa yeye ndiye chanzo cha tatizo lile.
HITIMISHO
Hiyo ni baadhi ya mifano kuhusu jinsi swali au maswali linaweza kuwa funguo au nguzo ya tafakari.
Hivyo basi ili uwe mtu unayefanya tafakari zenye tija lazima uzingatie misingi au nguzo au funguo za tafakari, funguo mojawapo ni kujiuliza maswali.
Jiulize maswali mbalimbali kama vile;
Kwa nini unaishi maisha hayo?
Hatima ya hayo unayotenda ni nini?
Kwa nini uende unakotaka kwenda?
Nakadhalika.

0 Maoni