MAISHA BAADA YA KUOKOKA

 



Waefeso 2:1-5

Mambo nitakayokufundisha katika somo hili

1.      Maana ya kuokoka na faida za kuokoka

2.      Aina ya maisha tunayotakiwa kuishi baada ya kuokoka

3.      Ubatizo

Utangulizi

Kufuatana na kitabu cha Waefeso 2:1-5 Biblia inatuambia kuwa kabla hatujaokoka kuna aina ya maisha au kuna mfumo wa maisha tuliokuwa nao uliotokana na kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, kumfuata shetani na kufuata tama za miili yetu.

Kutokana na maisha hayo Mungu alituchukulia kama watu tuliopotea, watu tuliokufa na watu tulioasi kwa kuwa kila ambaye hajamwamini Yesu anachukuliwa kama mtu aliyepotea ndio maana Biblia inasema kila amwaminiye Yesu asipotee bali awe na uzima wa milele (Yohana 3:16)

MAANA YA KUOKOKA NA FAIDA ZA KUOKOKA

Baadhi ya maana za kuokoka

v  Kuokoka ni kufanywa kuwa mwana wa Mungu (Yohana 1:12)

v  Kuokoka ni kukubali kuishi maisha yanayompendeza Mungu au maisha matakatifu (Waefeso 2:10) (1 Petro 1:15-16)

v  Kuokoka ni kukubali kuwa tofauti kitabia, usemi na kifikira yaani kuwa tofauti na watu ambao hawajaokoka (Wakolosai 3:5-10)

v  Kuokoka ni kuzaliwa mara ya pili kwa namna ya kiroho ( 1 Petro 1:23)

Baadhi ya faida za kuokoka

v  Unafanyika kuwa mwana wa Mungu (Yohana 1:12)

v  Jina lako linafutwa kutoka kwenye kitabu cha hukumu na linaandikwa kwenye kitabu cha uzima (Ufunuo 20:11-15)

Kitabu cha hukumu ni kitabu chenye orodha ya majina ya watu wanastahili kutupwa katika ziwa la moto lakini kitabu cha uzima ni kitabu chenye orodha ya watu wanaostahili kuingia katika ufalme wa Mungu ndio maana Biblia inasema anayemwamini Yesu ahukumiwi (Yohana 3:18)

v  Unasamehewa dhambi zako zote ulizowahi kuzitenda hata kama ni kubwa kiasi gani (Zaburi 103:3)

v  Unahamishwa kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingizwa katika ufalme wa mwana wa pendo lake (Wakolosai 1:13) Yaani unakuwa na mamlaka dhidi ya nguvu zote za giza unakuwa na mamlaka ya kuweka mikono juu ya wagonjwa ili wapokee uponyaji, unakuwa na mamlaka ya kuyatoa majini au mapepo n.k (Marko 16:17)

v  Mungu anaingia ndani yako na kukufanya kuwa makao yake (Ufunuo 3:20)

 

AINA YA MAISHA AMBAYO TUNATAKIWA KUISHI BAADA YA KUOKOKA

Baada ya kuokoka kuna aina ya maisha ambayo tunapaswa kuyaishi kwa kuwa sisi ni viumbe vipya.

1.      Tunatakiwa kuwa tofauti na watu ambao hawajaokoka, yaani tunatakiwa kuwa na tabia, usemi, mitazamo, muonekano, vipaumbele tofauti na watu ambao hawajaokoka (Wakolosai  3:1-25)

2.      Tunatakiwa kuongozwa na Roho Mtakatifu na sio tamaa za miili, tama ya macho na kiburi cha uzima (Yohana 14:26)

3.      Tunatakiwa kuwaambia wengine habari za Yesu yaani kushuhudia wengine habari za Yesu (Mathayo 28:19)

Mbinu mojawapo ambayo ni rahisi ya kuhubiri injili ni kuwaeleza wengine jinsi Yesu alivyokuokoa, jinsi Yesu alivyokubadilisha, jinsi Yesu alivyokuponya, jinsi Yesu alivyokusaidia.

Hiyo ndio mbinu aliyoitumia mwanamke msamaria aliyekutana na Yesu pale kisimani, Yule mwanamke alikwenda kuwaeleza wengine habari za Yesu jinsi alivyoyafunua maisha yake, ushuhuda wa Yule mwanamke ulisababisha watu wengi wakaokoka au wakamwamini Yesu (Yohana 4:39-42).

4.      Tunatakiwa kutoa fedha zetu au michango mbalimbali ili wengine wafikiwe na habari njema za Yesu.

(Warumi 10:14-15)

Kuhubiri injili ni pamoja na kuwasafirisha wahubiri wa injili au kununua vyombo au vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhubiria injili.

5.      Tunatakiwa kudumu katika ushirika yaani uwe na mahali unakoabudu au uende kanisani ambapo utakutana na watu wengine waliokoka, tunatakiwa kudumu katika kuomba, kushiriki meza ya Bwana na kujifunza neno la Mungu hilo linakwenda sambamba na kuwa na Biblia yako kuhudhuria semina au mafundisho ya neno la Mungu pamoja na kusoma vitabu vilivyoandikwa na watumishi wa Mungu mbalimbali (Matendo ya mitume 2:42)(Wakolosai 3:16)

 

 

 

UBATIZO

Ubatizo una maana kuu mbili

1.      Maana ya kimwili

2.      Maana ya kiroho

Maana ya kimwili

Ni kuzamishwa ndani ya maji na kuibuka tena.

Maana ya kiroho

Ni kufa na kufufuka pamoja na Kristo (Waefeso 6:4-5)(Wakolosai 3:1)

Aina za ubatizo unatakiwa kubatizwa baada ya kuokoka

1.      Ubatizo wa maji  (Marko 16:16)(Mathayo 28:19)

2.      Ubatizo wa Roho Mtakatifu (Yohana 1:33)

Baada ya kuokoka unatakiwa kubatizwa kwa maji mengi ambayo utabatizwa na watumishi wa Mungu pia unatakiwa kubatizwa kwa Roho Mtakatifu . Kubatizwa kwa Roho Mtakatifu ni kujazwa na Roho Mtakatifu.

 

HITIMISHO

Baada ya kuona maana na faida za kuokoka nipende kukuambia kuwa kuna njia moja tu ambayo itakufanya kuokoka, njia hiyo ni kumkiri Yesu kwa kinywa chako kuwa Bwana na mwokozi wa ulimwengu na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu Baba alimfufua kutoka kwa wafu (Warumi 10:9-10)

9. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. 10. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

 

Ikiwa uko tayari kuokoka sema maneno haya

 

Mungu Baba nakushukuru kwa upendo wako kwa ajili ya ulimwengu, ninamkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa ulimwengu ninaamini kuwa Mungu Baba ulimfufua Yesu katika wafu, ninaomba unisamehe dhambi zangu zote nioshe kwa damu ya Yesu iliyomwagika pale msalabani kwa kuwa nimerejea kwako mimi niliyekuwa nimepotea, Asante Baba kwa kunisamehe na kunisafisha, asante kwa kuwa jina langu umeliandika kwenye kitabu cha uzima.

 

Baada ya kusema maneno hayo tayari umeokoka, nami nitapenda kuwasiliana nawe ambaye umeokoka, tuwasiliane kwa namba za simu ­_+255767955334 au +255625775243

Chapisha Maoni

0 Maoni