MAMBO BAADHI YATAKAYOKUFANYA UFIKIE MAFANIKIO UNAYOYATAKA

Faraja Gasto

Utangulizi
Kila mtu anapenda kufanikiwa ila shida ya kutofanikiwa inasababishwa na mambo mbalimbali, ili ufanikiwe lazima ukabiliane na mambo hayo.
Unaweza ukajiuliza mafanikio ni nini?
Mafanikio ni kutimiza jambo fulani au kupata kile ulichotarajia kupata. Kwa mfano kama ulikuwa na malengo ya kupata gari ukalipata hayo ni mafanikio.
Mafanikio yapo ya aina mbalimbali kutegemeana na Nyanja za maisha ya mwanadamu, unaweza ukafanikiwa kujenga nyumba ila ukawa haujafanikiwa kupata gari, unaweza ukafanikiwa kupata nyumba na gari lakini ukawa haujafanikiwa kufahamika katika kata nzima, wilaya, mkoa au taifa.
Ukimuuliza kila mtu akuambie anataka maisha yake, au biashara yake au huduma yake iweje baada ya muda fulani, kila mtu atakuambia nataka niwe mfanyabishara mkubwa (ikiwa anafanya biashara), nataka niwe muimbaji mkubwa (ikiwa ni muimbaji), nataka niwe mtumishi mkubwa (ikiwa ni mtumishi). Lakini kusema “nataka niwe hivi na hivi” haijatosha kukufanya uwe hivyo, yapo mambo mengine ya kuzingatia ambayo yatakufanya uwe hivyo unavyotarajia kuwa.

1.Jifunze kutumia ulichonacho au tafuta maarifa (ELIMU)
Shida kubwa walionayo watu wengi ni kutojua namna ya kutumia walichonacho; nafasi ya kiuongozi, fursa, kutumia watu walio karibu nao, kutumia fedha ndogo walizonazo n.k. Kwa mfano unapotaka kuwa Rais wa nchi lazima uzijue sifa za Rais, namna ya kuwa Rais n.k
Kuna uhusiano mkubwa kati ya “mafanikio na ufahamu” huwezi kujua namna ya kutumia ulichonacho kama kama haujajifunza, kuna watu wana vitu vingi vya kuwatoa hatua moja kwenda nyingine lakini HAWAJUI NAMNA YA KUTUMIA HIVYO VITU. Ukisoma maandiko utaona ilifika wakati Musa akawa anamlilia Mungu lakini Mungu akamwambia “una nini” akasema nina fimbo, kumbe fimbo aliyokuwa nayo ingeweza kutumika kutatua changamoto lakini hakuwa anajua mpaka Mungu alipomuambia tumia hiyo fimbo ndio maana nakuambia ni muhimu upende kujifunza.
Ukisoma Biblia utaona wakati Mungu anampa kazi Yoshua ya kuwapeleka wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani, Mungu alimwambia “Kitabu cha torati kisiondoke kinywani mwako, yatafakari yaliyoandikwa na ukatende sawasawa na yote yaliyoandikwa maana ndipo UTAKAPOIFANIKISHA NJIA YAKO na ndipo UTAKAPOSITAWI SANA (Yoshua 1:8)
Mungu alimwambia cha kwanza ni KUJIFUNZA ili apate UFAHAMU wa yaliyoandikwa humo kwenye kitabu kutegemeana na kazi aliyopewa.
Cha kujifunza ni kwamba haijalishi unataka ufanikiwe katika eneo lipi JIFUNZE mambo mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali waliofanikiwa katika eneo hilo.

2.Tumia muda vizuri
Kuna uhusiano kati ya mafanikio na muda, kama haujui namna ya kutumia muda wako vema ni vigumu kufanikiwa. Usipojua namna ya kutumia muda utajikuta umekuwa mtu ambaye hauna msimamo, utajikuta umekuwa rafiki wa kila mtu hata ambaye hana mchango chanya kwenye maisha yako pia utajikuta haujui linalokupasa kufanya katika wakati fulani. Waulize wakulima huwa hawalimi maadamu wana mbegu au maadamu wana uwezo wa kulima, huwa wanalima zinapofika nyakati za mvua.

Mambo yatakayokufanya utumie muda wako vema
(a)Jifunze kujiwekea ratiba ya kila siku (TO DO LIST)
--Ratiba ya chakula, ratiba ya kubadilishana mawazo na ndugu, jamaa au marafiki, ratiba ya masuala ya kiroho (ibada n.k), ratiba ya kazi.
(b)Heshimu hiyo ratiba kwa kufanya kila ulichopanga kwa wakati.
(c) Zifahamu nyakati na majira, itakusaidia kufahamu kipi unatakiwa kukifanya kwa nyakati hizo na majira hayo.

3. Malengo
Kuna uhusiano kati ya malengo na mafanikio. Malengo ni pale unapotaka kufika (kituo) mafanikio ni kufika ulipotaka kufika (kufika kwenye hicho kituo).
Kwa hiyo unataka ufanikiwe katika eneo fulani jifunze kujiwekea malengo kwamba “baada ya miezi ……….. au mwaka mmoja au miaka ………. Nataka niwe mtu wa aina fulani”

4.Jiwekee mikakati
Ukishamaliza kujiwekea malengo, weka mikakati itakayokufanya uyafikie malengo hayo.
Mikakati ni namna utakavyofanya jambo ulilolikusudia. Kwa mfano kama mtu ni mwanafunzi na anataka kupata alama nzuri darasani lazima ajiwekee mikakati ya kusoma kwa bidii.
Vivyo hivyo katika eneo lolote unalotaka kufanikiwa lazima ujiwekee mikakati. Kama hauna mikakati basi sahau suala la mafanikio.


Chapisha Maoni

1 Maoni

  1. Yes , ahsante kwa makala pendwa na nzuri Mr Faraja Gastor

    Pia mafanikio yamebebwa ns
    1 kujiamini
    2, kujitoa means kuamua
    3: kupoteza ,nilazima ukubali kutumia pesa, muda na kuachana na marafiki wasio na faida
    By Simfukwe Gastor

    JibuFuta