HOJA ZENYE NGUVU (MAOMBI)




(Isaya 41:21)
Watu wengi wanamuomba Mungu lakini ni watu wachache wanaopeleka hoja zenye nguvu mbele za Mungu ndio maana watu wengine wamekuwa na maombi ambayo hayana majibu.
Nikupe mfano huu, wazazi wengi huwapatia watoto wao matakwa yao kulingana na hoja wanazokuja nazo kwa wazazi wao kwa mfano jaribu kufikiri mzazi ambaye ana watoto wawili; mmoja akaja kumuomba mzazi wake hela ili akanunue daftari na mwingine akaja kumuomba mzazi wake hela ili akatembee pamoja na mrafiki zake, kati ya hawa watoto wawili unahisi ni nani ambaye atajibiwa ombi lake kwa haraka?
Hoja zenye nguvu maana yake ni sababu zenye nguvu zinazomfanya Mungu akupe kile ambacho unakiomba kwake.
Kuna namna ya kibiblia ya kutengeneza hoja zenye nguvu ili unapokwenda mbele za Mungu kuomba hoja zako ziwe na nguvu na hatimaye Mungu ajibu maombi yako.

1.Mjue Mungu
Watu wengi wanajikuta wakiwa hawana majibu ya maombi sababu mojawapo ni kutomjua Mungu. Nataka nikuonyeshe jambo lililofanya maombi ya Musa yakapata kibali mbele za Mungu
(Kutoka 32:7-14)
Kilikuwa ni kipindi ambacho wana wa Israeli waliabudu ndama na kwa kufanya hivyo hasira ya Bwana ikawaka juu yao na Bwana akataka kuwaangamiza, lakini Musa alikwenda mbele za Mungu na hoja yenye nguvu(sababu iliyomfanya Mungu aghairi alichokuwa amekusudia kukifanaya) kwa kuwa Musa alimjua Mungu ni Mungu ashikaye maagano kutokana na hilo Musa alimwambia Mungu “Kwa nini wamisri waseme kuwa Mungu aliwatoa Misri ili apate kuwaangamiza” na pia Musa akamwambia Mungu “kumbuka uliahidi kuwa utauzidisha uzao wa Ibrahimu ili uwe kama mchanga wa Bahari sasa kwa nini uwaangamize hawa watu?”, Mungu aliposikia hoja hiyo ya Musa, Mungu alighairi kuwaangamiza kwa kuwa kuna hoja yenye nguvu ililetwa na Musa na ikasababisha Mungu aghairi alichokuwa amekikusudia, Mungu alighairi kuwaangamiza si kwa sababu waliomba msamaha ila ni kwa sababu Musa alijua kuwa Mungu anashika maagano na kwa kuwa aliahidi kuwa atauzidihsa uzao wa Ibrahimu ndio maana Musa alikwenda mbele za Mungu kwa ujasiri na hoja yake ikawa na nguvu mbele za Bwana.
Ni vema unapokwenda mbele za Mungu kuomba uwe na ufahamu juu ya kile ambacho Mungu ameahidi juu ya hicho unachotaka kuomba kwa kuwa Mungu analiangalia neno lake ili apate kulitimiza (Yeremia 1:12) ndio maana Musa alimwambia Mungu akumbuke kile alichomuahidi Ibrahimu na Isaka na Yakobo juu ya uzao wao na Mungu aliposikia alijibu yale maombi kwa haraka sana.

2.Mkumbushe Mungu (Ahadi zake au mambo mema uliyotenda)
(Kutoka 32:7-14)
Wakati ambapo Mungu ametaka kuwaangamiza wana wa Israeli kutokana na kuabudu ndama, Musa alimkumbusha Mungu kuhusu alichowahidi Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Mungu aliposikia kuhusu hilo ghafla akaamua kughairi kile alichokuwa amekusudia kuwatenda.
(Isaya 38:1-8)
Mfalme Hezekia alipougua na akawa kwenye hatari ya kufa alikwenda mbele za Mungu kuomba, hoja yake ilikuwa na nguvu kwa kuwa alimkumbusha Mungu juu ya mambo ambayo aliyatenda katika taifa alililiongoza, Mungu aliposikia hoja hiyo ghafla akamwambia Hezekia kuwa amemsikia na amemuongezea miaka kumi na mitano.
Unapokuwa na jambo la kumkumbusha Mungu hilo jambo linaifanya hoja yako unayopeleka mbele za Mungu inakuwa na nguvu na Mungu anakuwa tayari kujibu maombi yako?
Unapotenda jambo jema unajiweka ukumbusho mbele za Bwana (Matendo ya Mitume 9:36-41) unapotoa sadaka zako unajiwekea ukumbusho mbele za Bwana (Matendo ya Mitume 10;1-4) na kwa kuwa Mungu huwa ana kitabu cha ukumbusho (Malaki 3;16) unapomkumbusha Bwana kuhusu uliyotenda hoja hiyo inakuwa na nguvu mbele za Bwana na Mungu hawezi kukuacha jinsi ulivyo.

Chapisha Maoni

1 Maoni