KUJAA ROHO MTAKATIFU - Seh ya 4 Mwisho


 
MAMBO BAADHI YATAKAYOKUFANYA KUWA MKRISTO ULIYEJAA ROHO MTAKATIFU KILA WAKATI 

1. Kaa kwenye neno la Mungu (Matendo ya mitume 1:4-5)

Wanafunzi wa Yesu waliambiwa wasitoke Yerusalemu mpaka wabatizwe kwa Roho Mtakatifu, walitii neno hilo walikaa Yerusalemu, Roho Mtakatifu aliwakuta Yerusalemu akawajaza.

Kitendo cha wanafunzi wa Yesu kukaa Yerusalemu kilikuwa ni kitendo cha utii, walitii alichosema Yesu.

Ikiwa unataka kuwa mkristo uliyejaa Roho Mtakatifu kila wakati lazima ukae katika neno la Mungu, lisome, litafakari pia litendee kazi.

2.Tamani kujaa Roho Mtakatifu (kiu - Isaya 44:3). 
Kiu humfanya mtu kutaka kupata kitu fulani cha kimwili au cha kiroho. Kiu iliyoko ndani ya mtu huvuta vitu vingi vya kiroho haijalishi vinatoka kwa Mungu au kwa shetani kutegemeana na aina ya kiu iliyomo ndani ya mtu, Yesu alisema Mathayo 5:6.

Ukiwa na kiu ya kujaa Roho Mtakatifu, Bwana YESU atakujaza sana.

3. Kuwekewa mikono na mtumishi wa Mungu ambaye Mungu amekuweka chini yake (Matendo ya Mitume 9:17)

Njia hii ni njia mojawapo inayoweza kukufanya kuwa mkristo uliyejaa Roho Mtakatifu ila nashauri usikimbilie kuwekewa mikono kwa ajili ya ujazo wa Roho Mtakatifu kama Roho Mtakatifu hajasema na wewe au kama amani ya Kristo haijaamua hivyo moyoni mwako.

4. Usimzimishe Roho Mtakatifu (1 Wathesalonike 5:19)

Kumzimisha Roho Mtakatifu ni kumzuia asifanye jambo fulani au ni kuzuia jambo fulani la Roho Mtakatifu ndani yako au kutokea ndani yako.

Kwa mfano unajisikia kupaza sauti kusema jambo fulani halafu unajizuia, Elisabeth alijazwa Roho Mtakatifu akapaza sauti (Luka 1:41-42). 

Kwa mfano wakati mwingine Roho Mtakatifu humuwekea mtu msukumo wa kuomba, kutoa sadaka, kumpa mtu fulani kitu nakadhalika, ukiacha kutenda anachotaka Roho Mtakatifu unakuwa umemzimisha.

👉👉👉Yako mambo mengi yanayoweza kukufanya kuwa mkristo uliyejaa Roho Mtakatifu kila wakati, nimefundisha hayo machache yakusaidie.

Chapisha Maoni

0 Maoni