UTANGULIZI
Dunia inafundisha mambo mengi kuhusu maisha pia neno la Mungu linafundisha mambo mengi kuhusu maisha. Yale ambayo dunia inafundisha kuhusu maisha yanawachanganya watu sana na watu wengi hawajui maisha ni nini hasa.
Kwa mfano utasikia watu wakisema tunakwenda mahali fulani kutafuta maisha, au utasikia wengine wakisema fulani ana maisha mazuri, au utasikia watu wakisema fulani amepoteza maisha, au mtu anasema maisha ni magumu, au fulani amepata maisha nakadhalika.
Ila ukiwauliza watu wengi kuhusu maisha ni nini si ajabu ukasikia majibu tofauti kabisa.
TAFSIRI MBALIMBALI KUHUSU MAISHA
Kwa mujibu wa kamusi ya merriam Webster wanatafsiri maisha kama ni kipindi ambacho mwanadamu, wanyama na mimea kinaishi.
Kwa mujibu wa kamusi ya Cambridge wanasema ni kipindi kati ya kuzaliwa na kufa au ni kuwa hai.
Kwa mujibu wa kamusi ya Oxford wamesema mambo mengi kuhusu maisha jambo mojawapo wanasema maisha ni hali inayotofaitisha viumbe hai na visivyo hai.
Kwa mujibu wa kamusi ya Collins wanasema maisha ni hali ya kuwa hai.
Kwa mujibu wa mtandao wa Britannica wanasema maisha ni uwezo wa kukua, kubadilika nakadhalika.
BIBLIA INAFUNDISHA INASEMA NINI KUHUSU MAISHA
Neno maisha limetajwa kwa mara ya kwanza kwenye kitabu cha Mwanzo 3:14
MAANA YA MAISHA
MAANA YA KWANZA
Ni muda wa kuwepo kwa viumbe duniani (maisha ni muda wa kuwepo duniani)
Rejea baadhi ya maandiko kuhusu maisha (Mwanzo 3:14)(Mwanzo 3:17)(Mwanzo 7:11)(Mwanzo 25:7)(Mwanzo 25:17).
Maandiko yote hayo yanathibitisha kuwa maisha ni muda wa viumbe hai kuwepo duniani.
MAANA YA PILI
Maisha ni uhai au roho kuwa ndani ya mwili (Yakobo 2:26a)
Biblia inasema mwili pasipo roho umekufa, kwa hiyo watu wanaposema fulani amepoteza maisha maana yake ni kwamba roho imetoka ndani ya mwili.
MAANA YA TATU YA MAISHA
Maisha ni hali ya kiroho, kimwili, kijamii, kitabia au kiuchumi aliyonayo mtu au waliyonayo watu.
Hali kama ni nzuri huwa tunasema fulani ana maisha mazuri, kama hali ni mbaya mara nyingi tunasema fulani ana maisha mabaya au maisha magumu.
(Kutoka 1:13-14) Wamisri walihakikisha waisraeli wanakuwa na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii, hali mbaya ndicho ambacho watu wengi huita imaisha magumu.
(Amosi 5:4-6) Mungu anawaambia waisraeli kwamba "wamtafute nao wataishi" kumbuka kwamba anawaambia watu ambao wako hai kwamba wataishi, unaweza kujiuliza anasemaje wataishi wakati wao wanaishi (wako hai).
Alimaanisha kwamba kwamba wakimtafuta watapata hali nzuri ya kiroho, kimwili na kiuchumi.
HITIMISHO
Biblia ndio kamusi ya maisha, chochote unachohitaji kufahamu kuhusu maisha, Biblia imekielezea vizuri sana.
Chukua hatua, soma Biblia.

0 Maoni